Wagombea Ubunge 49 wapitishwa na INEC Temeke

DAR-ES-SALAAM : WAGOMBEA wa Ubunge 49 wamepitishwa kugombea nafasi hiyo katika majimbo matatu yaliyopo Wilayani Temeke, Dar es Salaam baada ya kukidhi masharti ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC). Majimbo hayo yaliyopo wilayani Temeke ni Temeke, Chamazi ambalo ni jimbo jipya na Mbagala.
Akizungumza na HabariLEO juzi, Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo hayo, Fortunata Shija alisema wagombea waliochukua fomu kwenye majimbo hayo yote walikuwa 51. Alisema mgombea mmoja wa jimbo la Mbagala na la Chamazi walishindwa kurejesha fomu za uteuzi na kufanya idadi kubaki 49.
“Katika Jimbo la Mbagala wagombea 17 walichukua fomu za uteuzi lakini mgombea mmoja wa Chama cha Makini hakuweza kurudisha fomu na kuifanya idadi ya walioteuliwa kuwa ni 16,” alisema na kuongeza: “Mwingine wa Jimbo la Chamazi kutoka UDP hawakuweza kurejesha fomu za uteuzi hivyo idadi ya wagombea inakuwa 15,” alisema.



