Wagombea Urais UDP na ufafanuzi wa Ilani UDP

KAMPENI za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa zinaendelea kuelekea siku ya uchaguzi Oktoba 29, 2025. Wagombea wa vyama mbalimbali walianza mchakamchaka Agosti 28, 2025 na kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kampeni zitahitimishwa Oktoba 28, siku moja kabla ya uchaguzi.

Miongoni mwa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo ni Chama cha United Democratic Party (UDP). Chama hicho na kimemteua Saum Hussein Rashid kuwa mgombea urais, huku kikimteua ni Juma Khamis Faki kuwa mgombea mwenza.

Katika kampeni za UDP, wagombea hao wanaahidi mambo mbalimbali, yakiwamo yanayohusu maendeleo ya kilimo, viwanda, afya, elimu na maji. Saum anasema chama chao kikichaguliwa na yeye kuwa rais, serikali yake itajenga kiwanda kila mkoa kadiri ya rasilimali zilizopo, ili kuinua uchumi na kuzalisha ajira kwa Watanzania.

Anasema UDP inatambua maendeleo ya viwanda ni kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi, ajira kwa vijana, kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje, kuongeza pato la taifa na kuimarisha mnyororo wa thamani wa rasilimali za ndani. SOMA: UDP yaahidi viwanda kila mkoa

Anasema UDP kinalenga sera ya viwanda itakayojikita kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, madini na ufugaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Lengo lingine ni kuweka miundombinu rafiki kwa uwekezaji wa viwanda ikiwamo ya umeme wa uhakika, barabara, bandari, sera thabiti za kodi pamoja na kushirikisha sekta binafsi kwa kutoa motisha na mikataba yenye usawa kwa wazawa na wawekezaji wa nje.

Anasema uwekezaji katika viwanda unalenga kujenga uchumi wa viwanda unaosukumwa na malighafi za ndani na kwamba, kilimo kitatoa msingi imara wa uzalishaji wa malighafi zitakazotumika katika kuchakata bidhaa mbalimbali.Anasema hatua hii inalenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kupanua fursa za ajira, kuongeza mapato ya serikali kupitia ushuru wa bidhaa zilizoongezwa thamani na kukuza uwezo wa taifa kwa kuuza bidhaa zilizochakatwa badala ya kuuza malighafi.

“Tumefanya utafiti wa haya na yanawezekana, yanatekelezeka. Tunaomba ridhaa yenu wananchi Oktoba 29, 2025 mtupigie kura, ili mabadiliko haya ya kiuchumi yawasaidie Watanzania wote na hasa wanyonge,” anasema Saum.

Kuhusu kilimo anasema, sera ya kilimo ya UDP inalenga kuinua ustawi wa kilimo kwa njia endelevu, jumuishi na rafiki kwa mazingira ili kuhakikisha usalama wa chakula, lishe bora, kipato kwa wananchi na mchango mkubwa kwa pato la taifa.

Sera inalenga kukabiliana na changamoto za uzalishaji, upatikanaji wa chakula, mabadiliko ya tabianchi na matumizi bora ya ardhi. Kwa mujibu wa mgombea urais huyo, ilani ya uchaguzi ya UDP inaainisha malengo makuu, ambayo ni kuimarisha uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara kwa kutumia teknolojia bora, pembejeo sahihi na umwagiliaji.

Anasema kilimo kimepewa kipaumbele, kwa kuwa kinatoa ajira kwa zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania na ndicho uti wa mgongo wa ukuaji wa uchumi mijini na vijijini. Anasema kilimo kina uwezo mkubwa kupanua wigo wa kodi kupitia ongezeko la uzalishaji, hivyo kuwezesha serikali kumudu gharama za mishahara ya watumishi wa umma. Kwa msingi huo, kukifanya kilimo kuwa injini kuu ya mapambano dhidi ya umaskini na msingi wa uchumi shindani unaojitegemea.

Afya bora Anasema, UDP inaamini kwamba afya ni msingi wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. “Sera yetu ya afya inalenga kuimarisha huduma bora za afya, kuongeza upatikanaji wa huduma hizo kwa wote na kuwekeza katika kinga, matibabu, mazingira bora, lishe, elimu ya afya na ushirikiano wa sekta mbalimbali ili kujenga jamii yenye afya njema na yenye tija,” anasema.

Malengo mengine anasema ni kupitia upya utafiti na takwimu katika sekta ya afya, ili kuweka msingi wa uboreshaji unaoendana na mahitaji halisi ya wananchi. Aidha, kuweka mkazo kwenye huduma za afya za msingi, upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na maslahi ya watumishi wa afya pamoja na kuweka mfumo wa bima ya afya kwa wote utakaofadhiliwa na serikali na mchango wa jamii.

Afya inapewa kipaumbele cha pili baada ya kilimo, kwa kuwa hakuna kilimo chenye tija bila afya bora kwa wakulima na jamii kwa ujumla. Elimu bora Saum anataja kipaumbele kingine kuwa ni elimu kwa kujenga taifa la watu wenye maarifa, ujuzi, maadili na elimu jumuishi ya kisasa.

Anasema kupitia sera na ilani, serikali ya UDP itaondoa vikwazo vyote vya kijamii, kiuchumi na kijiografia vinavyokwamisha watoto kupata elimu. Kwamba malengo makuu ni kupitia mfumo mzima wa elimu, kuanzia msingi hadi elimu ya juu kwa kuzingatia ufanisi wa mitaala, mazingira ya kujifunzia na walimu.

Mengine anasema ni pamoja na kuboresha elimu ya ufundi stadi na kuwekeza katika sayansi na teknolojia, ili kuhakikisha elimu inakuwa nyenzo ya ukombozi, ubunifu na ujenzi wa taifa. Anasema elimu ni kipaumbele cha msingi kinachotakiwa kutekelezwa kwa umakini na kwa hatua endelevu, kwa lengo la kupitia upya mfumo mzima wa elimu kuanzia ngazi ya msingi hadi elimu ya juu.

Kwa mujibu wa Saum, hatua hiyo inalenga kuandaa vijana wa Kitanzania kuwa washindani katika soko la ajira la kisasa na kwamba, mabadiliko hayo yamepangwa kutekelezwa kama kipaumbele cha tano. Maji safi na salama kwa wote Kipaumbele cha sera ya maji chama hicho kikiingia madarakani, Saum anasema ni pamoja na uwekezaji mkubwa katika upanuzi wa miundombinu ya maji, kuongeza mabwawa, mitambo ya kuchakata na kusambaza maji.

Vipaumbele vingine ni uhifadhi na ulinzi wa vyanzo vya maji, kuanzisha sheria kali za kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji, uchimbaji wa visima virefu vya kisasa na matumizi ya teknolojia rafiki. Anaseme bila maji safi na salama, hakuna afya ya jamii.

“Hakuna kilimo cha uhakika, hakuna viwanda vya kuchakata bidhaa, hakuna hifadhi ya mazingira, hakuna usawa wa kijinsia na maendeleo jumuishi,” anasema. Anasema kipaumbele hicho kinalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi, salama na ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani, kilimo, mifugo, viwandani na huduma za kijamii mijini na vijijini.

Aidha, kinalenga ujenzi wa miundombinu ya kudumu ya maji, kujenga mabwawa, visima, mitambo ya kuchuja maji, matenki, mabomba na mifumo ya umwagiliaji ya kisasa. Malengo mengine ni usimamizi endelevu wa vyanzo vya maji kuhifadhi na kulinda mito, maziwa, chemchemi na maji ya chini ya ardhi, ili yasikauke wala kuchafuliwa.

Lingine ni usawa wa kijinsia na kijamii katika huduma za maji, kuhakikisha wanawake, watoto na makundi maalumu wanapata kipaumbele, kutokana na athari kubwa wanazokumbana nazo kwenye uhaba wa maji. Matumizi ya teknolojia na ubunifu. Saum anasema UDP itachochea matumizi ya njia bunifu kama uvunaji wa maji ya mvua, teknolojia za kuchuja na kuhifadhi maji pamoja na mifumo ya kidigiti ya kusimamia matumizi. Naye Faki anawahimiza Watanzania kuzingatia kuwa, uchaguzi si ugomvi wala si vita, bali njia ya demokrasia kwa watu kuchagua viongozi wanaowataka kwa ajili ya maendeleo yao.

Kwamba, hata baada ya uchaguzi kuna maisha. Hivyo, Watanzania wasikubali kushiriki lolote linalotishia amani na usalama nchini. Kwa mujibu wa Faki, Tanzania ina amani na itaendelea kuwa nchi ya amani na ndiyo maana yanapotokea machafuko hata katika nchi jirani, wengi hukimbilia Tanzania.

“Ndugu zangu wa Morogoro, twendeni tukapige kura kwa amani. Tukumbuke kuna maisha baada ya uchaguzi,” anasema na kuongeza kuwa, katika kujitokeza kwa Watanzania wakiwemo wa Mkoa wa Morogoro, wakichague UDP. Anasema waasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume waliweka mifumo mizuri katika nchi.

“Walisema kila baada ya miaka mitano Watanzania wawe na uwezo wa kubadili viongozi kwa kuchagua wanaowafaa na kwa mantiki hii, niwaombe Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura,” anasema. Kwamba, baada ya kupiga kura kila mmoja arudi nyumbani au mahali pake pa kazi kwa amani na kuiacha INEC itangaze wagombea walioshinda.

Faki anahimiza Watanzania kuvitunza vitambulisho vya kupiga kura na kutokubali kurubuniwa na mtu yeyote anayetaka kuvichukua kwa nia ovu. Kwa upande wake, mgombea wa udiwani katika Kata ya Mji Mpya mkoani Morogoro, Salum Mwanduke anaelezea vipaumbele atakavyosimamia kama atachaguliwa kuwa diwani. Anavitaja kuwa ni pamoja na kusimamia mikopo ya asilimia 10 iwafikie walengwa bila upendeleo wala ubaguzi, uboreshaji wa miundombinu, huduma za maji pamoja na usafi wa mazingira.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button