Wagonjwa 17 wa moyo wafanyiwa upasuaji

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Shirika la Open Heart International la Australia, wamefanikiwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa 17 wa Kitanzania.
Wataalamu wa Open Heart International wapo nchini kwa kipindi cha siku 14 ambapo kati ya wagonjwa waliotibiwa, 13 ni watoto na wanne ni watu wazima. SOMA: Magonjwa ya kinywa yatajwa kuathiri moyo
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge amesema kuwa Open Heart International imekuwa ni moja ya washirika wakubwa wa taasisi hiyo, na hadi sasa wameitembelea JKCI takribani mara 14 tangu ilipoanzishwa.
Dk. Kisenge amelipongeza shirika hilo kwa kujitolea na kujituma katika kuokoa maisha ya Watanzania, akisisitiza kuwa uhusiano huo mzuri unatokana na juhudi za serikali katika kuimarisha uhusiano na serikali ya Australia. “Serikali imechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha mafanikio haya. “Tunashukuru kwa hilo. Uhusiano huu umewezesha upatikanaji wa vifaa tiba bora na msaada mkubwa kwa JKCI,” amesema Dk. Kisenge.

Akiendelea kueleza, alisema tangu taasisi hiyo ilipoanzishwa mwaka 2015, Open Heart International imekuwa ikifanya ziara kila mwaka na takribani watoto 200 wametibiwa hadi sasa. “Open Heart imefanya upasuaji mwingi na kuokoa maisha ya watoto wengi nchini mwetu,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi kutoka Open Heart International, Dk. Darren Wolfers amesema wanajivunia kuwa na nafasi ya kuokoa maisha ya watu, hasa watoto barani Afrika. “Tunawajali sana watoto wa Afrika na tunajivunia kuokoa maisha na kurejesha tabasamu kwenye nyuso zilizopoteza matumaini. Tunathamini imani na matumaini ambayo watu wanaweka kwetu,” amesema Dk. Wolfers.
Aidha, Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa JKCI aliishukuru timu ya Australia kwa kujitolea kwao na pia akaipongeza timu ya JKCI kwa juhudi kubwa walizoonyesha kipindi chote cha kambi ya matibabu. “Tumeona timu yetu ikifanya kazi kwa bidii kuanzia madaktari bingwa hadi wauguzi Timu ya Australia haikufanya upasuaji pekee bali pia ilitoa mafunzo kwa wafanyakazi wetu. Tunawashukuru sana kwa hilo,” amesema.
Shirika la Open Heart International limejikita katika kushirikisha jamii mbinu bora za kitabibu kwa kuleta upasuaji wa kisasa, vifaa, mafunzo, na elimu ya jamii kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa. “Kile tunachofanya si kuokoa maisha leo tu, bali ni kubadilisha uwezo wa jamii kuokoa maisha kwa muda mrefu,” limesema shirika hilo kwenye tovuti yake.



