Wagonjwa 400 Comoro waingiza zaidi ya Sh bilioni 2

DAR ES SALAAM; JUMLA ya Wagonjwa 400 kutoka Visiwa vya Comoro wamepata matibabu ya kibingwa bobezi hapa nchini, ambapo matibabu hayo yameiingizia nchi kiasi cha Sh bilioni 2.
Hayo yamesemWa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge wakati akikabidhi taarifa ya kambi maalumu ya matibabu ya ubingwa bobezi wa magonjwa mbalimbali iliyofanyika visiwani humo kwa Waziri wa Afya, Jenista Mhagama jijini Dodoma.
Dk Kisenge ambaye alikuwa mratibu wa kambi hiyo, amesema katika kambi hiyo iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana waliona zaidi ya wagonjwa 2700.
“Mwishoni mwa mwaka jana tulienda visiwani Comoro kuwatibu wenzetu ambao wanatutegemea Tanzania kupata huduma za ubingwa bobezi, tukiwa nchini humo tuliwajengea uwezo wataalamu wao na kujenga ushirikiano baina ya hospitali zao na zetu,” amesema Dk Kisenge.
Amesema kambi hiyo ilishirikisha wataalamu kutoka JKCI, Hospitali ya Benjamini Mkapa , Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Aidha katika hatua nyingine JKCI na Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa matibabu ya ubingwa bobezi wa magonjwa ya moyo kwa kutumia uwezo wa wataalamu wa ndani ya nchi.
Makubaliano hayo yalisainiwa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma na Wakurugenzi watendaji wa hospitali hizo.
Dk Kisenge amesema ushirikiano uliokuwepo baina yao na BMH umesaidia kuimarika kwa upatikanaji wa huduma ya matibabu ya moyo hapa nchini.
“Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wamekuwa wakiwajengea uwezo wataalamu wa magonjwa wa moyo waliopo BMH kwa kufanya hivi upatikanaji wa huduma ya matibabu ya kibingwa ya moyo umeongezeka na kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa uharaka,” amesema Dk Kisenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa BMH ,Prof. Abel Makubi amesema ushirikiano wa BMH na JKCI ulianza miaka mingi iliyopita, lakini sasa hivi wameona wauweke katika maandishi.
“Tutaendelea kushirikiana katika kufanya tafiti za magonjwa ya moyo, kutoa mafunzo kwa wataalamu wetu na kubadilishana ujuzi wa kazi hii ikiwa ni pamoja na kufanya matibabu ya pamoja,” amesema Prof. Makubi.



