Wahitimu uhasibu wahimizwa maadili

DAR ES SALAAM: Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Jenifa Omolo, amewataka wahitimu wa taaluma ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini kuzingatia uadilifu na maadili ya kazi kwa kufuata miongozo ya kisheria, ili kuepuka vitendo vya rushwa na kuimarisha uwajibikaji serikalini na sekta binafsi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mahafali ya 47 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Omolo amesema maadili na uaminifu ndiyo msingi wa taaluma ya uhasibu, na kuyapuuzia kunaweza kudhoofisha taswira ya taaluma hiyo pamoja na kuathiri uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, Profesa Sylvia Temu, amewataka wahitimu kuhakikisha wanazingatia miongozo ya kitaaluma wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, akibainisha kuwa bodi haitasita kuwachukulia hatua watakaokiuka kanuni na taratibu.
Wahitimu wa programu hiyo, akiwemo CPA Vaileth Victus na CPA Jafar Ogaga, wameeleza dhamira yao ya kutumia ujuzi walioupata katika kusimamia hesabu kwa uadilifu na kufuata misingi ya sheria na kanuni.
Mahafali hayo yameongeza idadi ya wataalamu wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini, hatua inayotarajiwa kuimarisha usimamizi wa fedha katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi.