Wajasiriamali 1,142 wasajiliwa Geita

GEITA: MKOA wa Geita umefanikiwa kusajili jumla ya wajasiriamali 1,142 katika mfumo wa urasimishaji kwa ajili ya utoaji wa vitambulisho na utoaji wa mikopo ya asilimia saba iliyotengwa na serikali kuu

Ofisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Geita, Martha Kaloso ametoa taarifa hiyo katika kongamano la wajasirimali lililofanyika katika viwanja vya Maonyesho ya Nane ya Teknoloji ya Madini mkoani Geita.

Martha amesema miongoni mwao wajasiriamali waliolipia kitambulisho cha usajili ni 231 sawa na asilimia 20 pekee ambapo thamani ya malipo yao ni kiasi cha Sh milioni 4.62.

Amesema kati ya hao pia waliopata mkopo mpaka sasa ni wajasiriamali 54 kupitia mkopo wa asilimia saba unaotolewa na serikali kuu kupitia benki ya NMB ambao wamepatiwa jumla ya Sh milioni 124.

Amesema wanufaika wa mkopo huo ni makundi mbalimbali ikiwemo mama lishe waliopata sh milioni 6.6, machinga wakipata sh milioni 105, wajasiriamali wengine wadogowadogo wakipatiwa Sh milioni 133.

“Kama mkoa wa Geita tunaendelea kutoa shukrani zetu za dhati kwa Rais wa Jamhur ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha fursa hii inawafaikia wajasiriamali”, amesema Martha.

Katibu Tawala Msaidizi mkoa wa Geita, Idara ya Uchumi na Uzalishaji Dk Elfas Msenya ameiomba NMB kunyambulisha na kuweka wazi changamoto zinazowakumba wajasiriamali waliokosa mkopo ili wasaidiwe.

Msenya amekiri kuwa uwiano wa idadi ya waliosajiliwa na waliopata mkopo mdogo ambapo ni vyema wajasiriamali waendelee kujitokeza kwa uwingi kwani serikali imetenga Sh milioni 70 kila halmashauri.

“Nitoe maelekezo pia kwa wenzetu maofisa maendeleo ya jamii, ngazi ya kata na halmashauri waendelee kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanapata elimu ya kujisajili na wawahamasishe kujisajili.

“Wale ambao watakuwa wanakwamisha hili eneo la usajili kwa kweli serikali haitakaa kimya, niwaombe sana wawasaidie wajasiriamali wadogo ili wajiandikishe na kupata fursa inayotolewana serikali”, amesema.

Ofisa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Geita, Justine Katiti amewahakikishia wajasiriamali kuwa wamejipanga kuwapa muongozo rafiki wa kufanya biashara bila tatizo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button