Wakadiriaji Majenzi waaswa mabadiliko ya teknolojia

DODOMA; WAKADIRIAJI Majenzi nchini wametakiwa kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani, hatua itakayoongeza ushindani na mchango wao katika sekta ya ujenzi.

Rai hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonde, akimwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Aisha Salim Amour, wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa 31 wa Taasisi ya Wakadiriaji Majenzi Tanzania (TIQS) ulioambatana na semina ya mafunzo kwa wataalamu wa sekta ya ujenzi.

“Hii itawawezesha kuongeza ushindani, kujiamini katika kutoa huduma na kutoa mchango bora kwenye miradi ya ndani na nje ya nchi. Kwa ubobezi wenu, sekta ya ujenzi itapata mafanikio makubwa,” alisema Msonde.

Mkutano huo wa mwaka ukiwa na kauli mbiu “Kuongeza Ufanisi wa Sekta ya Ujenzi Kupitia Maboresho ya Sera, Ushirikiano wa Wataalamu na Ubunifu Endelevu”, umelenga kuimarisha taaluma hiyo na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa.

Dk Msonde alisema Serikali inatambua nafasi kubwa ya wakadiriaji majenzi katika kupanga, kushauri na kudhibiti gharama za miradi ya ujenzi, akisisitiza kuwa uadilifu na weledi ni nyenzo muhimu za kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana kwa wananchi.

“Utaalamu wenu katika mikataba na usimamizi wa thamani ya fedha unasababisha miradi kukamilika kwa wakati, kwa ubora unaohitajika na kwa gharama stahiki. Niwasihi muendelee kufanya kazi kwa kuzingatia viwango vya taaluma,” alisema.

Akitaja miradi ya kimkakati, Dk Msonde alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwashirikisha wakadiriaji majenzi katika utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo SGR, Bwawa la Julius Nyerere, barabara na majengo ya serikali.

Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa kupanua ushiriki wao katika miradi yote ya ujenzi wa miundombinu ili kuongeza tija na kupunguza gharama zisizo na msingi.

Alizipongeza taasisi za serikali zinazotumia wakadiriaji majenzi waliosajiliwa kama vile CAG, TAKUKURU, TANROADS, TARURA, NHC, SUMA JKT na TBA kwa kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi.

Dk Msonde pia alisisitiza ushirikiano wa TIQS na taasisi za ndani na nje ya nchi katika kujifunza teknolojia mpya, huku akibainisha kuwa Serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) ya mwaka 2023 ili kupanua wigo wa ushiriki wa wataalamu katika sekta ya ujenzi.

“Mabadiliko haya yataongeza ufanisi wa huduma zenu na kuongeza mchango wenu katika maendeleo ya taifa,” alisema.

Kwa upande wake, Rais wa TIQS, Bernard Ndakidemi, alisema ni muhimu taasisi za ujenzi nchini kutumia wataalamu wa ndani kwa kushirikiana na wenzao wa nje, ili kuongeza tija na kuimarisha weledi wa sekta hiyo.

“Tunaiomba serikali isisite kuajiri wataalamu hawa kwa wingi katika taasisi zake. Hii ni fani adhimu na inathaminiwa duniani kote,” alisema Ndakidemi ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wakadiriaji Majenzi Afrika (AAQS) – Kanda ya Afrika Mashariki.

Aliongeza kuwa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) inafanya kazi kubwa ya kusimamia na kusajili taaluma hizo kwa niaba ya Serikali, hatua inayolinda weledi na maadili ya wataalamu.
Hata hivyo, aliitaka Serikali kuendelea kuiunga mkono bodi hiyo kwa kuipatia rasilimali za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuzuia kuingiliwa na watu wasio na utaalamu, weledi na maadili.

“Bodi hii ni muhimu sana kuhakikisha wanaofanya kazi hizi wana vigezo vinavyostahili. Tunaipongeza kwa mafanikio makubwa waliyoyapata hadi sasa,” alisema.

Mkutano huo unatarajia kujadili mada muhimu zikiwemo maboresho ya sera, uanzishwaji wa sheria ya majengo, matumizi ya teknolojia, ushirikiano wa wataalamu na afya ya akili, ambapo wadau wametakiwa kuchukua hatua madhubuti kushiriki katika maboresho hayo ili sekta ya ujenzi iwe ya kisasa, shindani na yenye tija.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button