Wakandarasi waagizwa kufanya kazi usiku, mchana

KAGERA: WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewaagiza wakandarasi wanaotekeleza mradi wa kimkakati upatikanaji wa miji katika miji 28 wa Rwakajunju Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera kubadili utendaji wake kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuwawezesha wananchi  kupata huduma ya maji kwa wakati.

Ametoa agizo hilo leo Julai 25, alipofanya ziara maalumu  ya kukagua mradi wa kimkakati wa miji 28 uliopo kata Nyabiyonza Wilayani Karagwe Mkoani Kagera ikiwa ni sehemu ya kuangalia namna  mradi huo unavyoendelea .

Amesema  kuwa tayari serikali ya awamu ya sita ya  Rais Samia iliridhia kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo hivyo hakuna wakandarasi kuweka visingizio bali wachape kazi usiku na mchana ili kuwaondolea changamoto ya maji waliyokuwa nayo kwa muda mrefu  wananchi wa Wilaya hiyo kwani huo ndio mradi pekee ambao utawaepusha  na adha ya upatikanaji wa maji.

“Utendaji wa kazi lazima ubadilike kuanzia sasa  hakikisheni mnafanya kazi usiku wa mchana na mradi huu ukamilike mwezi septemba mwaka huu kama Ambavyo tunakusudia kwa sababu lengo la serikali  ni wananchi kupata maji Na kutumia muda wao kuzalisha,”amesema Aweso.

Amesema  kuwa pamoja na mradi huo kutumia fedha nyingi lazima wakandarasi washughulikie changamoto za vibarua ikiwemo kuwapa mikataba ili kupunguza adha za vibarua hao wanatumika Kuharakisha kukamilika kwa mradi.

Alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Karagwe kalanga Laizer kuhakikisha anasimamia  suala la vibarua ili vijana wasipate changamoto kupata maslai yao.

Aidha, amewasihi wasimamizi wa Mradi huo ambao ni mamulaka  ya Maji na usafi wa mazingira Bukoba  BUWASA kuhakikisha wanazingatia maagizo ya Rais Samia katika upande wa eneo la kutibu maji ili wananchi wapate maji safi salama na bora.

Mratibu wa mradi huo kutoka Buwasa  Magreth Nyanga alisema mradi huo wa maji  unagharimu zaidi ya Sh bilioni 60 ambapo ulianza kimkataba April 11, 2023 unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu.

Amesema kuwa mradi huo Kwa sasa umefikia asilimia 64 ambapo amemuhakikishia waziri juu ya usimamizi wa  kazi hiyo  kwa usiku na mchana ili uweze kukamilika na wananchi  wapate maji safi na salama kwa wakati.

Mradi huo utakapokamilika  unatarajia kunufaisha maelfu ya  wananchi wa vijiji 13 kutoka Wilaya ya Karagwe  mkoani Kagera

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button