Wakazi Mkuranga walia kuvamiwa maeneo yao

PWANI: WAKAZI wa Mkuranga mkoani Pwani, Francis Maigua na Adventina Rweyemamu wanalilia maeneo yao ya Mwanadilato lenye ekari 104 na Mwanambaya ekari 80 kuvamiwa na watu wanaochimba mchanga bila idhini yao.
Wakazi hao wamedai maeneo hayo wanayamiliki kihalali na wana hati lakini wanashangazwa na watu hao kuyavamia kana kwamba ni ya kwao na baadhi yao wakiwa wameghushi hati na vibali vya uchimbaji.
Akizungumza na waandishi wa habari, Maigua amesema wameshaenda kuomba msaada kwa mamlaka mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga bila mafanikio.

Wanachotaka wakazi hao ni kurejeshewa maeneo hayo ili wao ndio wawe wasimamizi wa wachimba mchanga hao kwa mujibu wa sheria kwa kuwa ni wamiliki halali wa maeneo hayo.
“Tumesumbuka sana. Kuna watu wanatuletea vurugu, wanakuja na kusema sisi hatuna haki. Wakati sisi tuna vibali halali. Tumewahi kwenda kwa viongozi tofauti wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga , lakini bado hatujapata msaada,” amesema Maigua ambaye ni mume na wakili wa Adventina.
Hata hivyo, Dailynews Digital ilimtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Waziri Kombo kuuliza malalamiko hayo ambapo alisema suala hilo halijafika kwake lakini yupo tayari kukaa meza moja na wakazi hao kutafuta haki na Suluhu.
“Sina uhakika na hilo ila ninachojua ili uende ukachimbe mchanga katika eneo husika lazima uwe na vibali au barua kutoka kwenye Kijiji husika au uwe umewasilisha hati kwenye kijiji au mamlaka husika,
“Sikapokea hiyo kesi yao lakini waje tuongee tuone tatizo liko wapi, tufuatilie kwenye kijiji husika tuone haki itakuwa wapi,” alisema mkurugenzi huyo.
Awali, Maigua alisema yeye ni Mkenya na ameoa Mtanzania na wanaishi hapa nchini kwa miaka mingi na kwamba maeneo hayo anamiliki mke wake hivyo wanataka wayatumie kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo kuchimba mchanga wenyewe.



