Wakulima kunufaika ruzuku mbegu bora, pembejeo

MOROGORO: MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) inatarajia kusambaza mbegu bora za ufuta, pembejeo na viuatilifu kwa wakulima kuanzia msimu wa mwaka 2025/2026.
Kaimu Mkuu wa Kanda ya Mashariki wa Copra , Mary Majule amesema kwenye banda la Mamlaka hiyo katika maonesho ya Nane Nane ya Kanda ya Mashariki yanayofanyika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mkoani Morogoro ikishirikisha Mikoa ya Dar es Salaam,Tanga, Pwani na mwenyeji Morogoro.
Majule amesema zao la ufuta kwa sasa ni kinara katika kuingiza fedha nyingi ,hivyo hatua hiyo usambazaji huo kuwawezesha wakulima wapate mbegu bora zaidi ili kuongeza uzalishaji ufuta wenye viwango vya ubora.
Amesema imegudulika kuna changamoto ya mbegu hususani mbegu bora na wakulima kwani wengi wao wanalima kwa kutumia mbegu za kienyeji ambazo hazina ubora hasa katika soko la kimataifa.
“ Huu ni mkakati wa Mamlaka unaotarajia kufanyika kwa mwaka huu (2025) na zoezi litafanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, tayari tumeshapata mahitaji ya mbegu kwenye maeneo mbalimbali na vikao imefanyika na watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) “ amesema Majule.
Majule amesema lengo la kufanyika kwa vikao hivyo ni kujua ni namna gani Mamkala itapata mbegu ambazo zinafaa kwa ajili ya wakulima kwani mahitaji ya mbegu bado ni makubwa tofauti na uzalishaji wa sasa hivi.
“Kupitia utafiti na wadau wengine wanaozalisha mbegu Mamlaka itaongea nao ni kuona namna gani wataongeza uzalishaji wa mbegu ili ziweze kusambazwa kwa wakulima,”amesema Majule.
Majule amesema , Mamlaka inatengemea mbegu hizo zitakuwa zinatolewa kwa wakulima kupitia mfumo wa ruzuku na zitakapowafikia kwa wakati ni matarajio kuwa kadri miaka itakavyo kuwa inasonga mbele kutakuwepo na mbegu bora zaidi.
Kaimu Mkuu wa Kanda ya Mashariki wa Copra amesema kadri miaka itakavyokuwa inasonga mbele ukanda wa Mashariki hasa mkoa wa Morogoro utakuwa na ufuta wenye ubora zaidi kama ilivyo mikoa ya kusini hususani Lindi .
“Mkoa wa Lindi ufuta wao unapata bei kubwa zaidi kutokana na wakulima wanatumia mbegu bora zaidi ukilinganisha na mikoa mingine inayotumia mbegu za kienyeji,” amesema Majule.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo kuwa mazao yaliyoongoza kuingiza fedha kupitia mauzo ya nje na kuchangia pato la Serikali kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi 2025 ni pamoja na zao la ufuta ambalo limeingiza zaidi ya sh. trilioni 2.2 baada ya kuuzwa kupitia mfumo wa stakabali za ghala.