Wakulima wa pamba ‘wanavyolia’ bei kupata tija

“HATA kama itatokea bei elekezi ya kununua zao la pamba kwa kilo moja itangazwe kuwa itanunuliwa kwa Sh 3,000, kama wakulima wataendelea kuwa wabishi kukataa kulima kitaalamu, kuzalisha kwa tija, hawawezi kunufaika.”

“Tatizo kubwa ambalo tunalo kwenye sekta hii ya pamba ni ubishi kwa wakulima, hawataki kubadilika, hawataki kufuata utalaamu katika uzalishaji wa zao hili, tukiendelea kuwa wabishi, tukakataa utalaamu maisha yetu hayatabadilika.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Marco Mtunga anasema wakati akizungumza na wakulima wa zao hilo katika Mtaa wa Mwakibuga mkoani Simiyu, hivi karibuni. Anasema huo ndio ukweli ingawa wachache miongoni mwao na wakiwamo baadhi ya viongozi wa kisiasa, hawapendi kuyasikia.

Anasema ili wakulima wa pamba wabadilike na kubadilisha maisha yao dhidi ya umaskini na kuachana na malalamiko ya bei kila mwaka. Kwa mujibu wa Mtunga, kwa sasa kilimo ni sayansi hivyo, ni muhimu wakulima kusikiliza na kufuata maelekezo ya wataalamu ili wakulima wa zao hilo wafikie malengo yao.

Takwimu za Bodi ya Pamba Tanzania zinabainisha kuwa, nchini Tanzania kuna wakulima zaidi ya 600,000 katika mikoa 17, wilaya 56 na halmashauri 64 zinazozalisha pamba nchini wanaojihusisha na kilimo cha zao pamba. Mei 2, 2025 Serikali ilitangaza bei elekezi ya ununuzi wa zao hilo kwa msimu mpya wa 2025/2026, ambapo kilo moja ilitangazwa kununuliwa Sh 1,150 kwa pamba ambayo ni daraja la kwanza.

Bei hiyo iliyotangaziwa katika Mtaa wa Mwakibuga, Halmashauri ya Mji wa Bariadi, ilitangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Kenani Kihongosi kwa niaba ya serikali, huku pamba daraja la pili ikitangazwa kununuliwa Sh 575.

Kwa mujibu wa wakulima hao, bei iliyotangazwa hivi karibuni haina tofauti na bei iliyotangazwa mwaka jana
katika msimu wa ununuzi wa 2024/2025 ingawa baadaye ilipanda hadi kufikia Sh 2,000 katikati ya msimu wa
ununuzi.

Wakulima
Hata hivyo, bado kilio cha wakulima ni kile kile kila mwaka, baada ya bei kutangazwa wengi waliikataa wakitaka iongezwe hadi kufikia Sh 2,000 kwa kilo moja jambo ambalo limeendelea kuwa mjadala hadi sasa.

Kwa mujibu wa wakulima, bei ya Sh 1,150 kwa kilogramu moja haiwezi inawafanya wasioone tija ya kilimo cha zao hilo. Wanasema hiyo inatokana na kila wanachoita gharama kubwa wanayotumia katika uzalishaji ikiwemo ya kukodi mashamba vibarua kwa ajili ya nguvukazi.

Mmoja wa wakulima wa Mwakibuga, Buya Buluba anasema gharama wanazotumia hadi pamba kufikia hatua ya kuvunwa ni kubwa na kwamba, haiwezi kufidiwa na bei hiyo iliyotangazwa. Anasema, “Ukianzia katika kupata shamba wengi tunakodi tena kwa gharama kubwa, kuliandaa shamba kwa trekta ni gharama pia, lakini kubwa zaidi ule muda wa palizi tunalipa vibarua.”

Buluba anasema bei iliyotangazwa haiwezi kuwakomboa dhidi ya umaskini na wala hawawezi kunufaika nayo hivyo anaomba iongezwe hadi kufikia Sh 2,000. “Hii bei ambayo imetangazwa kusema kweli haitoshi hata kidogo tunatumia gharama kubwa kulima, tunawaomba warudi wakapange upya bei angalau waanzie Sh 2,000,” anasema Buluba.

Mkulima mwingine wa wilayani Meatu, Joseph Kitula anasema bei iliyotangazwa haiwapi ukombozi wa kiuchumi wala kijamii. “Tunaomba serikali ituonee huruma iongeze bei hadi walau Shilingi 2,200,” anasema Kitula.

Kwa mujibu wa Kitula, ni vizuri bei ya kuanzia iwe kubwa kuliko kuwategemea wanunuzi wa pamba ndio waongeze bei katikati ya msimu jambo analosema linawaumiza wakulima. “Bei ni ndogo sana hii, huu utaratibu wa kutangaza bei ndogo halafu unategemea matajiri (wanunuzi) ndio wapandishe katikati ya msimu unatunyonya sisi wakulima,” anasema.

Mkulima mwingine, Viale Madeleke anasema anaridhika na bei iliyotangazwa akiamini kuwa, itapanda kabla msimu wa ununuzi haujaisha. “Tumezoea kutangaziwa bei ndogo, lakini kadri msimu wa ununuzi unavyoendelea bei imekuwa ikipanda,” anasema Madeleke.

Anaongeza: “Katika msimu wa mwaka jana ilipanda hadi Shilingi 2,000 na awamu hii tunayo imani kuwa bei itapanda.” Asilimia kubwa ya wakulima wa zao hilo bado wanaendelea na mjadala wa bei iliyotangazwa. Wengi wanasema walau bei ya Sh 2,000 kwa kilogramu moja itawaondoa katika tishio la kuendesha kilimo cha pamba kwa hasara.

Watalaamu
Hata hivyo licha ya wakulima wenyewe kuhitaji hivyo, watalaamu wa zao hilo wanasema hata wakulima wakipewa bei ya Sh 3,000 hawawezi kunufaika ikiwa wataendelea kukataa utalaamu katika kilimo cha pamba. Kwa mujibu wa Mkurugezi TCB, Marco Mtunga, zao la pamba linakabiliwa na changamoto kubwa mbili.

Anazitaja kuwa ni tija ndogo katika uzalishaji pamoja na ubora wa pamba wakati wa kuvuna na kutunza. Anasema changamoto hizo zikitatuliwa, hakuna mkulima atayelalamikia bei kuwa ni ndogo, bali wakulima watajikita zaidi katika tija na ubora wa zao hilo. Anasema wakulima wengi wanazalisha kilo 100 hadi 300 kutoka katika shamba ya hekari moja.

“Mkulima anayezalisha hivyo hawezi kunufaika na zao hili hata kidogo na ndiyo wengi wanalalamikia bei,” anasema. Mtunga anaongeza: “Mkulima analima shamba la hekari 10, kisha anazalisha mafurushi 10, yaani kila hekari anatoa furushi moja, huyo mkulima ataendelea kulalamikia bei kila mwaka kwani uzalishaji wake uko chini sana.”

Anasema kutokana na hali hiyo, serikali kupitia TCB inaendelea kuboresha mazingira ya kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa tija kwa kuongeza maofisa ugani na kuleta teknolojia mbalimbali. Anasema mbali maofisa ugani, wakulima wamekuwa wakipata mbegu za kutosha bure, viuatlifu bure, lakini pia serikali imeleta ndenge nyuki zinazonyunyizia mashamba bure.

“Sasa hivi tumeleta mashine zile kubwa (trekta) za kunyunyuzia mashamba makubwa, ndio maana tumeweka nguvu zaidi wakulima walime kwa kufuata kanuni, tunataka kila mkulima azalishe kuanzia kilo 1,000 hadi 1,500 kwa hekari moja,” anasema.

Mtunga anasema katika msimu uliopita 2024/2025, mkulima namba moja Tanzania alitoka katika Wilaya ya  Chato ambaye katika hekari moja alikuwa anavuna kilo 2,750 na kwamba, alilima hekari tatu pekee. “Tunataka wakulima wengi zaidi wapunguze maeneo ya kulima, lakini wazalishe kwa tija; tunataka wakulima waache ubishi, wakubali sayansi, wafuate kanuni ndio watanufaika na hili zao,” anasema Mtunga.

Kuhusu changamoto ya pili katika zao hilo ambayo ni ubora, mkurugenzi huyo anasema baadhi ya wakulima wamekuwa wakichafua pamba hasa wakati wa kuvuna na kuitunza hali na mazingira yanasababisha bei kushuka. “Pamba yetu ya Tanzania ikipelekwa kwenye soko la dunia inashuka bei kwa sababu ya uchafu yaani inachafuka wakati wa kuvuna na wakati wa kutunza,” anasema.

Mtunga anasema maofisa ugani wamepewa jukumu la kuwasimamia wakulima na kuwapa elimu ya namna ya namna bora ya kuvuna na kutunza pamba isichafuke. Anawataka wakulima kubadilika, kuacha ubishi na kukubali matakwa ya sayansi ili kunufaika zaidi na kilimo cha pamba.

Anasema: “Kila mkulima achukue hatua, mtembelee mkulima anayefuata kanuni ujifunze na ubadilike”.

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. Kweli wakulima wa zao la pamba hawalimi Kwa tija.Elimu kuhusu zao la pamba izidi kutolewa,ila na bei iongezwe kwani kilimo Cha pamba kina changamoto nyingi kutokea shambani mpaka sokoni.

  2. Kweli wakulima wa zao la pamba hawalimi Kwa tija.Elimu kuhusu zao la pamba izidi kutolewa,ila na bei iongezwe kwani kilimo Cha pamba kina changamoto nyingi kutokea shambani mpaka sokoni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button