Wakulima wa tumbaku waahidiwa neema

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa serikali yake itaongeza kampuni za kununua tumbaku ya wakulima ili kuongeza ushindani na kuondoa adha ya kucheleweshewa malipo.

Ameahidi pia kuhakikisha fedha za wakulima wa tumbaku ambazo ni madai ya muda mrefu zinalipwa.

Akinadi sera za chama chake na kuomba kura kwa maelfu ya wananchi waliofurika Kata ya Ilolanguru
wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya kampeni, Samia amewahakikishia wakulima kuwa serikali bado ipo katika mazungumzo na Kampuni za PCL na Volecel ambazo hazijalipa fedha za wakulima.

“Niwahakikishie zitalipwa, kupitia Waziri wa Kilimo huwa ninataka ripoti kila baada ya muda aniambie mazungumzo yamefikia wapi ili wakulima walipwe fedha zao,” amesema.

Aliongeza: “Lakini nafurahi kusema tumeongeza kampuni za kununua tumbaku, sasa kuna ushindani na lile suala la mikopo na wakulima kuchelewa kulipwa fedha zao halipo tena, tutaendelea kufanya hivyo,” amesema.

SOMA: Samia aacha ahadi 4 Nyanda za Juu Kusini

Aidha, Samia ametumia fursa hiyo kuwapongeza wakulima wa tumbaku kwa kuongeza uzalishaji na kuwa hiyo imetokana hatua ya serikali yake kutoa mbolea na pembejeo za ruzuku.

Akizungumzia yaliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na ambayo serikali yake itatekeleza katika miaka mitano ijayo pindi atakapopata ridhaa ya kuunda serikali, Samia amesema walitekeleza ombi la watumishi katika sekta ya elimu.

“Ninafurahi tumeajiri walimu 412 ambao wameletwa ndani ya wilaya hii. Lakini na watumishi wa afya 161. Tunapoendelea mbele najua bado mahitaji ya watumishi yapo.” “Niliahidi ndani ya siku 100 mtakaponipa ridhaa kuendelea kuongoza nchi hii. Ndani ya siku 100 tutaajiri kwenye sekta ya afya watumishi 5,000 na walimu 7,000 bila shaka watafika na Uyui,” amesema.

Amesema katika sekta ya afya ndani ya wilaya hiyo serikali imepeleka Sh bilioni 8.2 ambazo zimetumika kuboresha huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya sita, zahanati mpya 17 na kuboresha hospitali ya wilaya.

“Nafahamu wilaya ni kubwa, hivyo mahitaji ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati bado yapo. Tumejielekeza kusaidia pale ambapo nguvu za wananchi zimeanza na serikali itakuja kumalizia,” amesema.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Samia amesema kuwa serikali imeongeza shule saba za sekondari hivyo kufikisha shule 34 kutoka 27 za awali huku idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 12,000 hadi 17,500.

Amesema pia serikali imeongeza shule za msingi 28 kutoka 124 hadi 182 na kuendelea kutoa elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.

“Tumejenga skimu za umwagiliaji zikiwemo Goweko na Unyanyama na kuendelea kutoa ruzuku ya mbolea, mbegu na dawa za chanjo kwa wafugaji. Tunapoendelea mbele tutaendelea na ujenzi wa majosho na mabwawa kwa ajili ya mifugo,” amesema.

Amesema kutokana na uwepo wa mahitaji kwa maeneo ambayo hayajapa maji, aliahidi kupitia mradi wa Ziwa Victoria ambao unatekelezwa serikali yake ikipewa ridhaa itajenga tangi lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni moja katika Kata ya Ilolangulu ambayo yatatumia na wananchi wa kata hiyo pamoja na kata za Kalola, Isila, Ndono na Mabama.

“Mwaka 2022 nilipokuwa hapa mlinieleza kuhusu uhitaji wa daraja la Mto Roya, sasa nataka niwajulishe tumekamilisha usanifu, michoro na gharama ya daraja hilo. Tumeshatenga fedha ndani ya mwaka huu wa fedha kwa hiyo tunatafuta mkandarasi ili daraja lianze kujengwa,” amesema.

Ametaja maeneo ambayo barabara za wilaya hizo zitakwenda kuboreshwa ni Ilolanghulu – Isenga – Kasisi A na
Ndono – Fuluma – Makazi.

“Kwenye sekta za maendeleo ya jamii, elimu, afya, umeme na majisafi na salama, serikali itakwenda na mwendo uleule, kwa sababu tunajua jinsi watu wanavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya huduma hizi yanaongezeka,” amesema.

“Tutafika mahali tunamaliza mahitaji ya umeme tutakapounganisha vitongoji vyote, tutakachobaki ni  kuunganisha kwenye majumba ya watu na huo utakuwa ni utashi wa watu,” amesema.

Aidha, Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa alihimiza umoja na mshikamano ndani ya chama ili kwenda kwenye uchaguzi wakiwa na nguvu kubwa ya ushindi.

“Ndugu zangu kazi imemalizika na wagombea wamepatikana, sifa ya CCM ni kurudi na kuwa chama kimoja ili twende kwenye uchaguzi kwa nguvu kubwa,” amesema.

Akiwa kwenye mkutano wa kampeni Urambo mkoani Tabora, Samia aliahidi kuliinua zao la tumbaku na kutafuta masoko ya ndani na kimataifa ya zao hilo.

Ameahidi pia kutekeleza miradi inayokwenda kuinua sekta ya kilimo na ufugaji ili kuinua uchumi wa wananchi wa Urambo na Kaliua na taifa kwa ujumla.

Samia amesema juhudi zilizofanywa na serikali yake zimechangia kukua kwa uzalishaji wa zao la tumbaku kutoka tani 11,208 mwaka 2021 hadi kufikia tani 20,494 huku serikali ikifufua kiwanda cha tumbaku mkoani Morogoro ambacho kinaongeza thamani kabla ya kusafirisha nje.

Pia, mapato ya wakulima yameongeza kutoka dola za Marekani milioni 11 mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 50 kwa mwaka 2024/2025, huku bei ya tumbaku ikipanda kutoka Dola moja kwa tani na kwa sasa Dola 2.5 kwa tani.

“Hivyo uzalishaji na mapato yake yameongezeka kwa asilimia 100… niwahakikishie tukipewa ridhaa tutafanya kila linalowezekana kulitengeneza zao la tumbaku na kutafuta masoko mazuri zaidi. Wito wangu kwa wana Tabora kupunguza kukata miti, tunakwenda kwenye teknolojia mpya ya kukausha tumbaku ili Urambo na Tabora yetu itunze mazingira yake yatakayosaidia kuwa mvua za kutosha na kupata maji ya kutosha kwa ajili ya kilimo na shughuli zingine,” amesema.

Samia amesema pia serikali yake itakwenda kujenga shule mpya 12 za msingi na sekondari. Kwenye sekta ya kilimo, alisema atakwenda kujenga soko la mazao na kujenga skimu mbili za umwagiliaji. Pia, serikali yake itajenga soko jipya na vibanda vya biashara katika stendi kuu ya mabasi.

Aidha, Samia amewahimiza wanawake ndani ya CCM, kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kutafuta kura za mgombea wa urais ambaye ni mwanamke.

“Kwa miaka yote wagombea urais wanatolewa na jumuiya ya vijana na jumuiya ya wazazi. UWT (Umoja wa Wanawake wa CCM) haikuwahi kutoa mgombea urais, huu ni mwaka wa kwanza kwa UWT kutoa mgombea urais. Kuanzia sasa wanawake tufunge kitenge kiunoni, viatu mguuni twende tukasake kura za mgombea wa UWT,” amesema.

KALIUA
Aidha, akiwa kwenye mkutano wa kampeni katika Wilaya ya Kaliua, Samia amesema ilani ya uchaguzi kwa wilaya hiyo inawaelekeza kuendeleza ujenzi wa vituo vya afya takribani vitano, zahanati nane na nyumba za watumishi.

Amesema pia kuhamasisha upimaji wa viwanja na kumilikisha kwa wananchi kwa viwanja vya makazi na biashara na kutaja barabara kadhaa zitakazojengwa kwa kiwango cha lami.

Samia pia ameahidi kwenda kujenga mabwawa na skimu za umwagiliaji za Konanne, Igombe, Mnange, Limbula na Igwisi na kuanzisha mradi wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT) katika sekta za kilimo na mifugo.

Pia, ameahidi kutekeleza mradi wa chujio la kutibu maji ya Bwawa la Ichemba sambamba na uchimbaji visima ili kuhakikisha vijiji vyote visivyo na maji katika wilaya hiyo vinapata huduma ya majisafi na salama.

Samia amesema pia serikali yake itaanzisha ranchi ya malisho na uhamilishaji mifugo, uanzishwaji wa minada, machinjio ya kisasa na majosho ya mifugo.

Ameahidi pia kukamilisha majengo katika Hospitali ya Wilaya ya Kaliua ikiwamo jengo la afya ya mama na mtoto.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button