Wakulima wadogo wafaidika na kilimo Ekolojia

MTANDAO wa wakulima Afrika Mashariki na Kusini (ESAFF) umesema umefanikiwa kuwafikia wakulima wadogo zaidi ya milioni tatu nchini Tanzania kupitia kilimo ekolojia, kwa kuwaunganisha kushiriki vikao vya kuibua vipaumbele, vikao vya bajeti na mafunzo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yalibainishwa jijini Nairobi na Meneja wa Programu wa ESAFF, Emanuel Justine, wakati wa warsha iliyokutanisha wakulima wadogo, wadau wa kilimo na waandishi wa habari kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema ESAFF inashirikiana na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kuhakikisha wakulima hao wanapata fursa za mafunzo, uragibishi wa sera na kushiriki katika maamuzi ya kisera yanayohusu sekta ya kilimo. SOMA: Viongozi mitaa watakiwa kutoa elimu ya mazingira

“Lengo la warsha hii ni kujifunza pamoja, kutathmini changamoto za wakulima wadogo na kuangalia namna tunaweza kushirikiana na vyombo vya habari kusukuma ajenda ya mabadiliko ya tabianchi kuanzia ngazi ya kijiji hadi kimataifa,” alisema Justine.

Uwekezaji katika kilimo ekolojia

Justine alisema kilimo ekolojia kikiwekewa uwekezaji wa kutosha kinaweza kuwa suluhisho endelevu dhidi ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Alieleza kuwa wakulima wadogo wengi wameshaanza kutumia mbinu hizo ikiwamo kuchanganya mazao, kutengeneza mbolea kutokana na samadi na taka za nyumbani.

“Ni muhimu mamlaka kutambua ukweli wa changamoto zinazowakabili wakulima wadogo na kufanya marekebisho ya sera yanayowaunga mkono. Hii ndiyo njia ya kuhakikisha wakulima wanaendeleza uzalishaji wa chakula,” alisisitiza.

Alibainisha kuwa wakulima wadogo huzalisha asilimia 80 ya chakula duniani, huku vyakula vya kilimo ekolojia vikiwa na uhitaji mkubwa katika masoko ya kimataifa. Hata hivyo, bidhaa zinazotumia viuatilifu na mbolea za kemikali hukataliwa katika baadhi ya nchi zilizoendelea.

Ushiriki wa kijamii na kiuchumi

Mbali na kushiriki katika vikao vya bajeti na kupanga vipaumbele, alisema wakulima wadogo kupitia MVIWATA wameanzisha vikundi vya akiba na mikopo (SACCOS), vinavyowawezesha kupata mitaji na kufanya biashara kwa pamoja.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Wakulima Afrika Mashariki (EAFF) kutoka Uganda, Elizabeth Msemadala, alisema mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuwa changamoto kubwa kwa wakulima barani Afrika kutokana na kilimo kutegemea zaidi mvua.

“Zaidi ya asilimia 80 ya kilimo chetu kinategemea mvua, lakini rasilimali za kusaidia wakulima hazifiki ipasavyo. Ndiyo maana tumeungana katika kampeni hii ya hatua za hali ya hewa kwa wakulima wadogo ili kuwa na sauti moja kimataifa,” alisema.

Msemadala aliongeza kuwa changamoto zinazowakabili wakulima Afrika zinatofautiana na zile za mabara mengine, hivyo ni muhimu kuweka mikakati mahsusi ya kikanda ili kuhakikisha sekta ya kilimo inakua na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button