SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Kanda ya Mashariki imewataka Viongozi wote wa umma kuzingatia matakwa ya katiba na sheria ya maadili ikiwa ni pamoja na kuwasilisha tamko la rasilimali na madeni la mwisho wa mwaka kabla ya Desemba 31,mwaka huu.
Katibu Msaidizi na Mkuu wa Kanda ya Mashariki ,Hendry Sawe ametoa rai kwa viongozi wa umma wa kanda hiyo kwa wale ambao hawajatekeleza tamko hilo kufanya hivyo kabla ya muda uliowekwa kwa mujibu wa sheria .
Sawe ametoa rai hiyo mjini Morogoro kwenye wiki ya kulelekea maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu kwa kanda hiyo ambayo inaundwa na mikoa ya Tanga na Morogoro.
Wiki ya maadhimisho hayo imeanza Desemba 5 ,mwaka huu ambapo kilele chake ni Desemba 10, mwaka huu.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu kwa mwaka 2024 ni : “Tumia haki yako ya kidemokrasia chagua Viongozi waadilifu na wanaozingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa maendeleo ya Taifa.
Amesema ,ikumbukwe kwamba kwa kuzingatia sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu cha 9(1)(b) kinamtaka kiongozi wa umma kila mwisho wa mwaka kabla ya Desemba 31,kuwasilisha tamko lake kwa kamishna wa maadili .
Sawe amesema ya kwamba , linapasa kuonesha rasilimali zake, au mume au watoto wake wenye umri usiozidi miaka kumi na minane (18) ambao hawajaoa au kuolewa.
“Napenda kuchukua fursa hii tena kuwakumbusha Viongozi wote wa Umma kuwa ni kosa kwa Mujibu wa Kifungu cha 16 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Kiongozi kushindwa kutoa tamko lake la rasilimali na madeni bila sababu za Msingi, “ amesema Sawe.
“…au, kuchelewesha kuwasilisha tamko la rasilimali na madeni bila kuwa na sababu ya msingi au kutoa Tamko chini ya fungu la 9 akijua ni la uongo au potofu katika kipengele chochote muhimu” amesisitiza Sawe.
Amesema fomu za tamko la rasilimali na madeni kwa sasa zinapatikana katika mtandao wa maadili (Online System).