PWANI; WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji mkoani Pwani, Mohamed Mchengerwa, ametoa Sh milioni 40 kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa mbegu kwa zaidi ya wakazi 1,000 wa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Rufiji ambao mali, mashamba na makazi yao yameathiriwa na mafuriko ya maji, yaliyofunguliwa kutoka Bwawa la Uzalishaji Umeme la Mwalimu Nyerere.
Akizungumza na wakazi hao mara baada ya kufanya ziara ya kukagua athari ya mafuriko hayo katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, Waziri Mchengerwa amesema analazimika kutoa kiasi hicho cha fedha ili kuwatia moyo wakazi hao kurejea shambani kulima upya, baada ya mazao yao kusombwa na mafuriko hayo.
“Hili ni janga letu sote mimi na nyinyi, tuliamini kwamba ujenzi wa JNHPP utakuwa mkombozi wa mafuriko ambayo yamekuwa yanatukumba mara kwa mara, lakini kwa bahati mbaya bado imejitokeza, tuendelee kuwa na imani kwamba mradi ukikamilika huenda changamoto hii ikawa imetatuliwa,” amesema Waziri Mchengerwa.
Ameongeza: “ Ninafahamu fika namna wakazi wa Rufiji mlivyokuwa mmelima kwelikweli mwaka huu, ninaomba turejee shambani tulime tena vilevile kwa kiwango kikubwa, mimi ninamkabidhi Mkuu wa Wilaya shilingi milioni 40 kwa kuanzia kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa mbegu, ili turejee shambani tupande tena tusije kufa kwa njaa.”
Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa taasisi na mashirika ya misaada ya kibinadamu pamoja na wasamalia wema kuguswa na hali ya Warufiji kwa kuwashika mkono kwa namna moja au nyingine katika kipindi hiki ambacho serikali ya wilaya inaendelea na ufuatiliaji na tathimini ya athari za mafuriko hayo kwa ujumla.
“Ukweli niseme kiasi hiki cha milioni 40 nilikuwa nimekidunduliza kutoka kwenye mshahara wangu kwa ajili ya kuhakikisha tunakuwa na futari ya pamoja katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan kama tunavyofanya kila mwaka, lakini kwa hali hii ya mafuriko niseme tu kwamba futari si kitu nalazimika kutoa kiasi hiki kwa ajili ya ununuzi wa mbegu na nitaenda kuwaomba marafiki zangu wanichangie angalau tufikishe milioni 100 kwa ajili ya kusaidia warufiji walioathirika na mafuriko haya,” amesema Waziri Mchengerwa.
Halima Mbwana mkazi wa Kijiji cha Chumbi ambaye ni miongoni mwa waathirika wa mafuriko hayo amedai kuwa hali inazidi kuwa mbaya kuanzia chakula, marazi na makazi na hivyo wanatamani kupata wasamalia wa kuwashika mkono.
“Tumesalia watupu, mazao shambani yamesombwa na maji na hata vyakula vya ziada tulivyokuwa navyo vimesombwa pia, nyumba nazo zimesombwa na maji sasa hatuna pa kuishi wala hatuna chakula, tunaomba tusaidiwe maana hali zetu ni mbaya kwakweli,” amesema Mbwana.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele tathimini ya awali imebaini kuharibiwa kwa nyumba 58, na jumla ya wakazi 951 waliokuwa wakiishi kwenye maeneo ya vitongoji vya Kanga, Kiegele, Kilindi na Nyandote katika Kata ya Chumbi wameondolewa katika maeneo yao na kuhamishiwa sehemu salama, huku zaidi ya hekta 28,374.74 za mazao ya kilimo na bishara kama vile mahindi, mpunga, ufuta na ndizi zikiathiriwa na mafuriko hayo.