Waliokufa ajalini Rombo wafikia 10

IDADI ya watu waliofariki katika ajali ya barabarani iliyotokea Rombo mkoani Kilimanjaro juzi alasiri, imefikia 10 baada ya abiria aliyekuwa amejeruhiwa katika ajali hiyo kufariki usiku wa kuamkia jana.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala amethibitisha kutokea kifo cha mtu huyo, katika ajali iliyotokea Kijiji cha Kibaoni, Tarakea wilayani Rombo.

“Huyo mtu wa kumi aliyefariki hakuwa mmoja wa abiria kwenye magari yaliyohusika kwenye ajali hiyo, bali alikuwa akipita njia kwa miguu ajali hiyo ilipomkuta ambapo alipelekwa Hospitali ya Huruma iliyo Rombo kupatiwa matibabu,” alisema Mwangwala.

Kifo cha mtu huyo kinafikisha idadi ya watu 10 waliokufa kwenye ajali hiyo iliyothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa.

Akithibitisha ajali hiyo, Kamanda Maigwa alisema ilitokea kwenye Barabara Kuu ya Moshi – Tarakea Kibaoni, Tarafa ya Tarakea saa tisa alasiri juzi.

“Ajali hiyo iliyotokea ilihusisha gari lenye namba za usajili T 620 DZQ basi aina ya Yutong mali ya Kampuni ya Ngasere lililokuwa limetokea jijini Dodoma, ambapo liligongana na gari dogo la abiria lenye namba za usajili T 959 CKU aina ya Toyota Noah ambalo lilikuwa limetokea Tarakea kuelekea Moshi,” alisema Kamanda Maigwa.

Aliwataja waliofariki ni Mamasita Lowassa (27), Damaris Mwikau (22), Peter Urio (38), Monia Mumbua (64), Eligatanasi Kanje (30) na Hilda Leberatus (24).

Alisema miili mingine minne haijatambuliwa, akiwemo wa 10 aliyefariki usiku wa kuamkia jana, wakati miili yote imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Huruma na kwamba Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi juu ya ajali hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button