Wamiliki famasi zingatieni weledi kulinda afya za wananchi

MAMLAKA ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) imeonya wamiliki wa maduka ya dawa muhimu kuacha uuzaji wa dawa ambazo haziruhusiwi kwa mujibu wa sheria, ikieleza kuwa hali hiyo ni tishio kwa usalama wa afya ya jamii.

Onyo hilo lilitolewa na Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa TMDA, Anitha Mshighati wakati wa kukabidhi shehena ya dawa zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 17 zilizotaifishwa na kukabidhiwa katika zahanati za Magereza na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) mkoani Njombe.

Kwa mujibu wa Anitha dawa hizo hakikupaswa kuuzwa katika maduka ya dawa muhimu. Kwa maana hiyo wamiliki wa maduka hayo wamekiuka sheria, miongozo na taratibu, na matokeo yake wamejisababishia hasara kwa bidhaa zao kutaifishwa na kufutiwa leseni.

Tunaungana na TMDA na kuwapongeza kwa hatua hiyo kwani ukiukaji wa sheria na miongozo hiyo kunaleta athari kubwa kwa wananchi wanaozitumia dawa hizo. SOMA: TMDA yatahadharisha matumizi holela ya Dawa

Tunajua ziko sheria na kanuni za kudhibiti utoaji wa dawa kama Sheria ya dawa za Kulevya, Sheria ya Usalama wa Chakula na Dawa na nyingine lakini baadhi ya wamiliki wa famasi hizo wameamua kuweka maslahi mbele bila kujali usalama wa watumiaji jambo ambalo husababisha madhara.

Tunajua kuuza dawa ambazo hazijapimwa, zimepitwa na muda au za bandia kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa watu, famasi zinazouza dawa bila kusajiliwa na kuzingatia maelekezo ya kitaalamu zinaweza kusababisha kuenea hata kwa magonjwa. Tunataka kuwakumbusha wamiliki wa famasi kuwa mbali na madhara kwa watumiaji lakini pia wanajipunguzia imani ya wananchi kwa sekta ya afya na huduma za famasi.

Tunaamini mkono wa sheria ni mrefu, hivyo serikali itahakikisha kuwa sheria za uuzaji wa dawa zinaheshimiwa na zinatolewa adhabu kali kwa wale wanaozivunja.

Lakini pia elimu zaidi inahitajika kwa wamiliki wa famasi na wafanyakazi ili waweze kuzingatia weledi kwa kufuata sheria na kanuni wanapotoa huduma. Ni matumaini yetu pia serikali kupitia taasisi na mamlaka zake itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika famasi hizi ambazo zimefunguliwa katika mitaa yetu ili kubaini na kuchukua hatua dhidi ya wale watakaokutwa wamekiuka sheria na miongozo.

Aidha, tunatoa rai kwa mamlaka husika kuona umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na jamii kwa ujumla kwani baadhi yao wamekuwa wakifika katika famasi kuchukua dawa na kushinikiza dawa wanazotaka bila kuzingatia walichoelekezwa na daktari au hospitali.

Tunaamini kila mmoja akiona umuhimu wa kulinda afya muuzaji dawa na mnunuaji tutaepusha madhara mengi na hatari kwa afya za wananchi. Ujenzi Bandari kavu Tunduma uongezwe kasi kutatua foleni.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button