Wamiliki migodi wapewa siku 30 kusajili miradi

RUVUMA: BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa siku 30 kwa wamiliki, waendeshaji wa migodi, vituo vya kuuzia na kuhifadhia makaa ya mawe kuhakikisha wanasajili miradi yao ili kupata vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na kuhakiki ndani ya siku 30 kuanzia Desemba 8, 2024.
Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria NEMC, Jamal Baruti ameeleza hayo kutokana na ukaguzi uliofanyika katika vitalu mbalimbali vya migodi na kubaini makosa yanayokiuka Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004.
Baruti amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Mkoa wa Ruvuma mara baada ya zoezi la ukaguzi kufanyika.

Ametaja makosa yaliyoonekana katika ukaguzi huo kuwa ni kutofanyika kwa tathmini ya athari za mazingira (TAM), ukosefu wa mifumo ya usimamizi wa mazingira na kutelekezwa kwa migodi pasipo kukarabati mazingira.
Vile vile uchafuzi wa vyanzo vya maji na hewa, kuongeza mawanda ya shughuli za migodi bila taarifa na idhini ya kisheria, kukosekana kwa taarifa za upelembaji za kila mwaka na kukosekana kwa mipango ya urejeshaji mazingira.
Amesema ukaguzi huo uliofanywa na timu ya wataalam kutoka NEMC kwa kushirikishana na wamiliki wa migodi umefanyika katika migodi 16 kati ya 18, maeneo ya biashara za makaa ya mawe saba kati ya 15 na maeneo mawili ya utafiti kuanzia Novemba 27 hadi Desemba name mwaka huu, 2024 katika Wilaya za Madaba, Songea, Nyasa na Mbinga mkoani Ruvuma.

Pia amesema timu hiyo ya ukaguzi imetoa elimu elekezi kwa wamiliki wa migodi ikiwemo kuweka miundombinu ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira, na ukarabati endelevu wa mazingira.
Amesema baraza litaendelea kutoa maelekezo na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wamiliki wa migodi ili kuhakikisha uzingatiaji wa Sheria na utekelezaji maagizo yaliyotolewa ikiwa ni pamoja na kutosita kuchukua hatua za kisheria kwa wadau wote watakaoshindwa kutekeleza maelekezo hayo.

Vile vile kupewa adhabu ama kusimamisha shughuli zao ili kulinda mazingira, afya ya jamii na kuhakikisha uwiano wa maendeleo ya kiuchumi, uhifadhi wa mazingira na rasilimali za taifa.



