“Wanachama AfCFTA watumie fursa kibiashara”

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji na Mwenyekiti wa Mkutano wa 13 wa Mawaziri wa Biashara Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afika (AfCFTA) amezisitiza nchi wanachama wa mkataba huo kutumia fursa zilizopo ili kukuza biashara.

Dk Kijaji ameyasema hayo Januari 30, 2024 alipofungua akifungua Mkutano wa 13 wa Mawaziri wa Biashara AfCFTA unaofanyika Durban, Afrika Kusini, mkutano huo unafanyika kwa siku mbili kuanzia jana na leo.

Amezitaka nchi hizo kuendelea kushirikiana katika kukamilisha Itifaki ya Uwekezaji, Itifaki ya Biashara ya Kidigitali, pamoja na majadiliano kwenye vigezo vya uasili wa bidhaa na kukamilisha masuala muhimu yanayohusu mifumo ya utatuzi wa migogoro katika ufanyaji biashara kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara.

Dk Kijaji amesema ushirikiano wa nchi  hizo kupitia AfCFTA utachangia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu ya usafirishaji wa barabara, reli na usafiri wa anga, usalama, ukosefu wa nishati ya kutosha, uzalishaji mdogo na mawasiliano.

Mkutano huo wa 13 wa mawaziri ulitanguliwa na mikutano kadhaa katika ngazi ya wataalam ikiwemo mkutano wa 16 wa Kamati ya Makatibu Wakuu pamoja na mkutano wa 10 wa masuala ya Kamati ya Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara  iliyofanyika Januari 23 hadi 29, 2024.

Habari Zifananazo

Back to top button