Wanafunzi 11,000 wadahiriwa NIT

DAR ES SALAAM: CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimesema hadi sasa kimefanikiwa kudahili wanafunzi 11,000 wenye sifa za kusoma katika taasisi hiyo.
Takwimu hizo zimetolewa Septemba 22,2025 na Mkuu wa Chuo hicho, Dk Prosper Mgaya, wakati wa ufunguzi wa bonanza la michezo lililoandaliwa ikiwa ni kuelekea kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
“Kwa kipindi cha nusu karne sasa, NIT imekuwa nguzo muhimu ya elimu ya usafirishaji nchini. Ni lazima ufaulu uwe wa kuridhisha ili kupata nafasi ya kusoma chuoni hapa. Safari hii, zaidi ya wanafunzi 2,000 walikosa nafasi kutokana na ushindani mkubwa,” amesema Dk Mgaya.

Katika maadhimisho hayo, chuo pia kilitangaza kuwa kimeingia makubaliano na Kampuni ya L Technics, inayojihusisha na masuala ya usafiri wa anga, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuongeza ubora wa mafunzo ya usafirishaji wa anga.
Kwa mujibu wa Dk Mgaya, mradi huo umesaidia NIT kupata vifaa vya kisasa vinavyokidhi viwango vya kimataifa kwa ajili ya mafunzo ya urubani, matengenezo ya ndege na huduma za ndani ya ndege. Alibainisha kuwa vifaa hivyo vimeidhinishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Afrika Mashariki (EAVA), jambo linaloiruhusu NIT kutoa mafunzo ya kimataifa.
“Kupitia makubaliano haya na L Technics, tutashirikiana kutoa mafunzo na kuhakikisha wahitimu wetu wanapata leseni zinazotambulika kimataifa. Pia tunajadili uwezekano wa kuanzisha mfumo wa digrii mbili ya ndani na ya nje ili wahitimu wetu wapate fursa kubwa zaidi ya ajira ndani na nje ya nchi,” ameeleza.

Aidha, amesema NIT itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu usalama barabarani ili kupunguza ajali, ambazo zimekuwa janga kubwa na kusababisha vifo vya zaidi ya Watanzania 18 katika mikoa ya Dodoma, Pwani na Mwanza.
“Mbali na elimu hiyo, tutafungua kituo cha ukaguzi wa magari. Ukaguzi huo utafanyika bure kwa wafanyakazi na watu wengine kutoka nje ya chuo. Magari yatakayokutwa na matatizo yatapewa ushauri pamoja na matengenezo, ili kuepusha ajali,” amesema Dk Mgaya.
Kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya NIT kinatarajiwa kufanyika mwishoni mwa Desemba, kutegemea ratiba ya viongozi wakuu wa serikali.



