Wanafunzi wa sekondari wataka amani uchaguzi

DAR ES SALAAM: Wanafunzi zaidi ya 200 kutoka shule mbalimbali za sekondari jijini Dar es Salaam wamekutana kwa mdahalo kuelekea Uchaguzi Mkuu, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani ili kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao.
Mdahalo huo uliandaliwa na Shirika la Vijana na Wanawake (TAFEYOCO), ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Elvis Makumbo, amesema lengo ni kuwajengea vijana uelewa kuhusu nafasi yao katika kulinda amani na kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa uchaguzi.
“Amani ikipotea, ni vijana ndio wa kwanza kuathirika. Tumeona ni muhimu kuwapa wanafunzi nafasi ya kujadili mustakabali wa taifa lao, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi,” amesema Makumbo.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Helen Kelvin, amesema kupoteza amani kutaleta athari kubwa kwa maendeleo ya taifa na maisha ya wanafunzi.
“Uchaguzi unaokuja utakuwa na mafunzo makubwa, tukipoteza amani hatutaweza kuendelea na masomo yetu. Nchi isiyo na viongozi bora hushindwa kusonga mbele,” amesema.
Goodluck kutoka Shule ya Sekondari Azania amesema amani ni nguzo ya taifa na jukumu la kila Mtanzania ni kuitunza.
“Tunawaasa Watanzania wenzetu kuheshimu haki ya kuchagua viongozi kwa amani. Tukikosa amani tutapoteza kila kitu tulichojenga,” amesema.
Naye Elsie Paul kutoka Shule ya Sekondari Jangwani amesema machafuko yameathiri elimu katika mataifa mengine na Tanzania inapaswa kujifunza kutokana na hali hiyo.
“Kwa mfano, wenzetu Sudan wamepoteza fursa za elimu kwa sababu ya migogoro. Tanzania imetoa hifadhi kwa wakimbizi wengi kutokana na amani yetu, tusiharibu sifa hiyo,” amesema.
Wanafunzi hao wamesema mabadiliko ya kweli hayawezi kupatikana kwa kumwaga damu bali kwa kuheshimu misingi ya kidemokrasia na kufanya uchaguzi wa amani.