Wanafunzi wapatiwa bima ya afya ya jubilee bure

ARUSHA: WANAFUNZI mkoani Arusha wamehakikishiwa huduma za matibabu baada ya kupatiwa Bima ya afya bure na Kampuni ya Jubilee Health Insurance pamoja na Jubilee Life Insurance.
Msaada huo uliotolewa Alhamisi wiki hii umewanufaisha wanafunzi 10 wa Shule ya Msingi Meru.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Jubilee Health Insurance, Dk Charles Wankomba ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Kitengo cha Uhusiano na Watoa Huduma alisema mpango huo ni sehemu ya dhamira ya Jubilee katika kuboresha afya, elimu na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Dk Wankomba alibainisha kuwa msaada huo unaendana na dhamira kuu ya kampuni hiyo ya kusaidia watu kuishi maisha yenye afya na usalama zaidi.
“Kwa kugharamia mahitaji ya afya ya wanafunzi hawa wadogo, Jubilee inalenga kuwajengea msingi imara zaidi kwa ajili ya elimu na maendeleo yao ya baadaye,” alisema.

Kwa upande wake, Dereck Rwezaura, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Jubilee Life Insurance, alisisitiza umuhimu wa upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watoto, akibainisha kuwa afya njema ni kichocheo muhimu cha ufanisi bora wa kielimu na mafanikio ya muda mrefu.
Alisema mpango huo unaonyesha dhamira ya Jubilee Insurance ya kurudisha kwa jamii na kuleta mabadiliko ya dhati katika maisha ya familia za Kitanzania.
Hatua hiyo pia inaimarisha nafasi ya Jubilee kama mshirika wa kuaminika katika mfumo wa huduma za afya wa taifa, kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma kwa sababu ya changamoto za kiafya.
Kwa mujibu wawakilishi hao, bima ya afya iliyotolewa kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Meru ni miongoni mwa miradi mingi inayotekelezwa na kampuni hiyo kusaidia jamii nchini kote.
Akizungumzia msaada huo, Rose Shewari kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha aliipongeza kampuni hiyo, akisisitiza kuwa baadhi ya watoto kutoka familia masikini walihitaji msaada huo kwa kiwango kikubwa.
“Nawashauri wazazi wa wanafunzi walionufaika wawe mabalozi wa bima ya afya kwa wazazi wengine ili kuhakikisha watoto wao pia wananufaika,” alisema Shewari.



