Wanahabari waagizwa kulinda taarifa binafsi

TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imeagiza vyombo vya habari vilinde taarifa binafsi za watu.

Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma PDPC, Innocent Mungy alisema hayo wakati akiwasilisha mada kwenye mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Dar es Salaam jana.

Mungy alisema ni muhimu waandishi wa habari waelimishane katika vyumba vyao vya habari kuhusu namna sahihi ya kulinda taarifa binafsi wanaporipoti habari.

“Watu wanapoenda kutafuta habari wajue ni namna gani ya kulinda taarifa binafsi za watu. Uliyemuhoji umwambie kwamba hizi taarifa zinaenda sehemu fulani ili aridhie,” alisema.

Mungy alishauri pia vyumba vya habari viwe na sera ya ulinzi wa taarifa binafsi ili kuwalinda wale wanaotoa taarifa.

“Kwenye vyombo vya habari hata kama ni mnaenda mubashara watu wanatakiwa wajue kwamba wanaenda mubashara na anayetoa taarifa ni lazima ahakikishiwe ulinzi na akikuambia hili usiliandike basi kweli utatekeleza hilo suala,” alisema.

Aliongeza kuwa faragha na ulinzi wa taarifa binafsi vinapaswa kuingizwa na kuwekewa msisitizo katika utendaji wa vyombo vya habari na kwamba wanahabari ndio wasimamizi wa hilo.

Pia, alihimiza waandishi wa habari wahakiki taarifa kabla ya kuzichapisha au kuzipandisha hewani kuepuka kuingia katika mitego ya kupotoshwa kwa picha au picha mjongeo zisizo halisi.

Mungy alisema kuelekea uchaguzi kutakuwa na taarifa nyingi za upotoshaji kutumia akili unde, hivyo utakuwa wakati wa vyombo vya habari kujijengea jina kwa kuhakikisha taarifa.

“Kuelekea uchaguzi vitu kama hivi vinakuwepo, vitu vya ajabu sana, usia wangu kwenu kila habari ya uchaguzi kama inahusisha picha iwe video, kuna ‘software’ (programu tumizi) ambazo zinafanya uhakiki kuhusu video kama ni ya kweli au si ya kweli. Hakikisheni kabla ya kutoa habari mnafanya uhakiki wa taarifa,” alisema Mungy.

Alisema akili unde inaweza kutumika vibaya kumpendelea mgombea au chama fulani kwa watumiaji wake kutengeneza picha na sauti zisizo halisi na kusababisha hasara kwa vyombo vya habari kuingia hasara ya kujisafisha baada ya kuripoti taarifa ya kupotosha.

Mkurugenzi wa Usajili na Uzingatiaji katika Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Stephen Wangwe alisema ni muhimu vyombo vya habari vikaungana na INEC na PDPC kuzielewa changamoto za ulinzi wa taarifa binafsi ili kuzitafutia ufumbuzi.

Aliongeza kuwa vyombo hivyo vinapaswa kuzingatia ulinzi wa taarifa binafsi ili kuepuka kwenda kinyume na demokrasia kuelekea uchaguzi mkuu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button