WANANCHI katika baadhi ya mitaa ya Manispaa ya Morogoro wamejitokeza siku ya kwanza ya kujiandikisha katika vituo vya wapiga kura kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 27,2024 .
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima ameongoza wananchi wa mtaa wa Liti ulipo kata ya Mlimani kujiandikisha katika daftari hilo leo, ambapo uandikishaji wake utafikia ukomo Oktoba 20 Mwaka huu.
Baada ya kujiandikisha RC Malima ameridhishwa na idadi ya wananchi waliojitokeza kuwa kubwa ikiwa ni siku ya kwanza.
“Ninawaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kuchagua viongozi wanaofaa”amesema Malima.
SOMA: Tamasha lahamasisha uchaguzi mitaa
Wakazi wa mtaa huo, Khadija Yusuph na Raila Rashid ambaye ni Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Cha Liti Morogoro kwa nyakati tofauti walifurahishwa na maandalizi ya uandikishaji wa uchaguzi huo.
Walitumia fursa hiyo kuhimiza wakazi wengine wa mtaa huo waweze kujitoleza kujiandikisha ili waitumie haki yao ya kikatiba ya kuchagua kiongozi wanayemtaka.
Mkoa wa Morogoro una vituo vya kuandikisha wapigakura vipatavyo 3,752 katika halmashauri za wilaya zote za mkoa huo .
Katika uandikishaji huo watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo wanawake wajawazito wanapewa kipaumbele wakati wa zoezi hilo .