Wananchi Olorieni wataka miradi ya maendeleo iharakishwe

ARUSHA: WANANCHI wa Kata ya Olorieni na Magaiduru zilizoko katika Jimbo la Ngorongoro mkoani Arusha wameeleza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi hao kutokana na jiografia ya eneo hilo, huku wakitoa wito kwa serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi muhimu ya maendeleo katika jimbo hilo.

Wametoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanywa na mgombea ubunge Jimbo la Ngorongoro aliyepita bila kupingwa, Yannick Ndoinyo alipokuwa akifanya ziara ya kumwombea kura Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Samia Suluhu Hassan katika kata hizo.

Miongoni mwa changamoto zilizotajwa ni pamoja na ucheleweshaji wa kukamilika kwa jengo la ofisi ya Mtendaji wa Kata, hali inayokwamisha utoaji wa huduma kwa wananchi, pamoja na ubovu wa miundombinu ya daraja linalounganisha kata hiyo na barabara Kuu ya Loliondo-Arusha kwani daraja hilo huathiriwa mvua za masika na kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii.

Aidha, wananchi hao wameiomba serikali kuunganishwa na mradi mkubwa wa maji unaopita jirani na eneo hilo, hususan katika Kitongoji cha Lukumai ili na wao waweze kunufaika na mradi huo kwa kupata maji safi na salama kwa ajili ya binadamu na mifugo.

Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Sakara Murkuk alieleza kuwa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama limekuwa kikwazo kikubwa katika maisha yao ya kila siku na kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii.

Akijibu changamoto hizo katika kata za Olorieni, Maaloni na Malambo, Yanick Ndoinyo, aliahidi kushirikiana na serikali na wananchi kushughulikia changamoto hizo haraka iwezekanavyo mara tu atakapoapishwa kuwa mbunge.

Ndoinyo alieleza kuwa Ilani ya CCM imetambua na imepanga kutekeleza ujenzi wa barabara ya kilomita 164 kwa kiwango cha lami kutoka Kigongoni, Mto wa Mbu wilayani Monduli hadi Sale, Ngorongoro, hatua ambayo itafungua fursa za kibiashara na kurahisisha usafirishaji wa mazao na bidhaa.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, serikali imetoa zaidi ya Sh bilioni 88 kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo, na kwamba atahakikisha miradi yote iliyosalia katika ilani inatekelezwa kikamilifu.

Mbali na hayo, mgombea huyo ameahidi kuanzisha Benki ya Wananchi wilayani Ngorongoro ili kusaidia wakazi kuinuka kiuchumi, pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kusindika nyama, kitakachowezesha wafugaji kupata thamani ya mazao yao ya mifugo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro,Lucas Olemasiaya, alieleza kuwa lengo la mikutano hiyo ya hadhara katika kata za Jimbo hilo ni kuwaombea kura wagombea wa chama hicho kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Olemasiaya alisisitiza kuwa Serikali ya awamu ya tano imefanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 88, na kwamba chama hicho kitaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi iliyobaki kwa manufaa ya wananchi.

Mwananchi ,Lucas Kaisemi, mkazi wa Kata ya Maaloni katika Jimbo la Ngorongoro aliipongeza serikali na kueleza imani ya wananchi kwa CCM, huku akiomba changamoto ya malisho ya mifugo nayo itafutiwe suluhu ya kudumu ili wafugaji wa Jimbo hilo waweze kunufaika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button