Wananchi wa Mabira kunufaika na mradi wa maji

KAGERA: Wananchi zaidi ya 6,920 wa Kata ya Mabira wilayani Kyerwa mkoani Kagera wanatarajia kunufaika na huduma ya majisafi na salama pindi utakapokamilika mradi wa maji wa Mabira.

Ni katika mwendelezo wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mkoani Kagera ambao umeweka Jiwe la Msingi katika mradi huo uliofikia asilimia 98.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Kyerwa, Kashonele Kagodoro amesema kuwa mradi huo umegharimu zaidi ya Sh milioni  769.5 ambapo mpaka sasa Sh milioni 698.8 zimelipwa kwa mkandarasi na tayari wananchi wameanza kuunganisha maji katika majumba yao.

Amesema mradi huo utakamilika Novemba mwaka huu na upo katika matazamio ya mwisho ambapo wananchi wa kata hiyo walikuwa wanatembea kilometa 17 kufuata maji safi na salama.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ally Ussi  amewataka wananchi kutohujumu miradi ya maji na kutunza miundo mbinu ambapo amewaomba wananchi hao pia kujiunganishia maji katika nyumba zao ili kutumia muda mfupi katika maswala ya maji.

Amesema lengo la serikali ni kumtua mama ndoo kichwani hivyo vijiji ambavyo havijapata maji katika wilaya ya Kyerwa watapata maji safi na salama kupitia miradi inayotekelezwa na RUWASA.

“Nawapongeza RUWASA kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maji yenye viwango ,kwa sasa vijijini ni kama  mjini lengo la serikali ni kuhakikisha mwananchi anapata maji ndani ya mita 400 naamini kadri tunavyoendela kufikia mwaka 2030 wananchi wote watakuwa wamepata  maji,” amesema Ussi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button