Wananchi washauriwa kupiga kura

MWANZA: WAKAZI wa Mkoa wa Mwanza wametakiwa kutosusia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, bali wameshauriwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupiga kura.
Rai hiyo imetolewa jana na mgombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia ACT Wazalendo, Zitto Kabwe wakati wa mkutano wa mgombea ubunge wa chama hicho katika Jimbo la Nyamagana jijini Mwanza, Esther Thomas.

Kabwe amesema uchaguzi huu ni muhimu sana na hakuna namna yoyote tunaweza kuingia madarakani bila kupiga kura.
“Nimekuja mkoa wa Mwanza, kwa lengo mmoja tu kuwaombea kura wagombea udiwani na wabunge wa ACT Wazalendo waweze kuwaongeza na kuwaletea maendeleo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kabwe amesema endapo wakazi wa Nyamagana watamchagua mgombea wa ubunge wa jimbo la Nyamagana, ACT Wazalendo Esther Thomas watashirikiana naye katika kutatua tatizo la Wafanyabiashara wadogo.

Ameahidi kushirikiana na Esther ili kumaliza tatizo la wafanyabiashara wadogo kukosa eneo la kufanyiabiashara bali watatenga maeneo malumu ili wafanyabiahara waweze kutenga maeneo na mitaa ya kufanyia biashara.
Naye mgombea ubunge wa Jimbo la Nyamagana kupitia ACT Wazalendo, Esther Thomas amewaomba wakazi wa jimbo lake kumchagua ili aweze kuboresha sekta ya elimu, afya na uchumi.
Amesema atahakikisha analeta usafiri kwa wanafunzi pamoja na kuboresha miundo mbinu ya jiji la Mwanza ikiwemo mitaro na kuleta magari ya kufanya usafi kwajili ya kusafisha jiji la Mwanza.
Ameahidi kujenga maktaba ya kujisomea katika kila kata ili wanafunzi waweze kujisomea.



