Wananchi watakiwa kujitokeza kupima macho

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ,Geophrey Pinda,amewataka wananchi wa Jimbo la Kavuu mkoani Katavi,kujitokeza kwa wingi kupata huduma ya macho na mkojo ili kuimarisha afya zao na kuendelea na shughuli za uzalishaji.

Pinda ametoa kauli katika hafla ya uzinduzi wa kambi ya wiki mbili kwa ajili ya matibabu hiyo.

Pinda amesema ataendelea kuboresha huduma za afya katika hospitali hiyo kwa kuongeza vitendea kazi vya kisasa ikiwa ni kuunga jitihada za serikali kupitia tuzo ya ‘The Gates Goalkeepers Award’kama kielelezo cha matokeo makubwa ambayo yamepatikana kwenye uongozi Samia Suluhu Hassan kufuatia ripoti ya utafiti wa demografia na afya ya mwaka 2022 inayoonesha kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 80.

Mratibu wa kambi hiyo kutoka Shirika la Ujerumani la Afrika Blindenhilfe, Irene Alma amesema wameamua kufanya kambi hiyo kutokana na kuwepo kwa wahitaji wengi wa huduma ya macho na upasuaji wa magonjwa ya mkojo ambao mara kadhaa wameshindwa kumudu gharama za matibabu hayo.

Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji wa magonjwa ya Mkojo, Said Mauji amesema timu ya wataalamu hao imebaini uwepo wa wagonjwa wengi wa matatizo ya njia ya mkojo ikiwemo tezi dume na hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya kambi ya matibabu iliyofanyika Novemba 2024.

Aidha baadhi ya wakazi wa mkoa huo wameishukuru serikali kwa kutoa huduma hiyo kwani imekuwa mkobozi mkubwa kwao, kwa matibabu ya kibingwa ambayo awali walishindwa kuyapata kutokana na gharama kubwa.

Ikumbukwe kuwa hii ni Kambi ya Pili ya Matibabu inafanyika jimboni hapo kambi ya awali ilifanyika Novemba 2024 huku zaidi ya wananchi 140 wakifanyiwa upasuaji wa huduma ya macho na kambi hii ya pili itajumuisha upasuaji wa magonjwa ya njia ya Mkojo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button