Wananchi watakiwa kushiriki uhakiki taarifa za anwani

VIONGOZI wa serikali za mitaa mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la uhakiki wa taarifa za anwani za makazi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kukuza uchumi wa kidigitali.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kilimanjaro, upande wa Miundombinu, Jackson Masaka, alipokuwa akimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa kwenye uzinduzi wa zoezi hilo katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

Advertisement

Zoezi hilo linalotarajiwa kudumu kwa siku 12 linahusisha halmashauri nne za mkoa huo ambazo ni Manispaa ya Moshi, Wilaya ya Moshi, Rombo, na Hai ambapo kabla ya uhakiki kuanza, kutakuwa na mafunzo ya siku mbili kwa wenyeviti wa mitaa na watendaji wa kata na mitaa ili kuwajengea uwezo wa kusimamia mfumo wa anuani za makazi.

“Tumieni mafunzo mtakayopata kuondoa changamoto ya majina ya barabara zilizopo katika maeneo yenu, kuna majina mengine ambayo bado yana migogoro, mhakikishe kila mwananchi anafahamu kutumia anuani za makazi na muendelee kuhuisha taarifa hata baada ya zoezi hili kumalizika” amesema Masaka

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Posta kutoka Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia, na Habari, Caroline Kanuti, amesema kuwa zoezi hilo ni muhimu na lilisaidia kubainisha makazi yaliyoathirika na maporomoko ya udongo Wilayani Hanan’g na mafuriko ya wilaya za Rufiji na Kibiti hivyo kurahisisha shughuli za uokozi na kurejesha miundombinu.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Tehama kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, Melkiori Baltazari, alisema mfumo huo unaweza kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kubainisha kuwa juhudi hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa R4 unaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe alisema zoezi hilo litaleta chachu ya maendeleo katika mitaa 60 iliyopo katika manispaa hiyo.