Wanasaikolojia watoa ‘tiba’ utulivu wa akili
WANASAIKOLOJIA nchini wameshauri jamii kutafuta utulivu wa kiakili kwa kutoka nje ya makazi yao ili kukutana na watu wengine na kuona namna hali ya usalama ilivyorejea jambo litakalowasaidia kuwa sawa kiakili.
Mwanasaikolojia kutoka Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (TAPA), Jesusa Malewo amewashauri watu watembee hadi kwenye maeneo ambayo walikuwa wanayaogopa ili kuona kile wanachofikiri hakipo na wakubaliane na hali ilivyo sasa.
Amewasihi wazungumze na watu mara kwa mara na kila mmoja afanye utambuzi kwa mwenzie ili kubaini kama tabia zao zimebadilika kwa ajili ya kuwasaidia kurejea katika hali ya mwanzo.
“Baadhi ya watu walishuhudia watu wakipoteza maisha, wapo ambao wameharibiwa mali na biashara zao, hivyo kutokana na hali hiyo baadhi yao wamepata majeraha ya kihisia, tatizo linaloweza kuwafanya wakumbuke mara kwa mara na kuwapa kiwewe kwa sababu utendaji kazi wa mfumo wa akili umebadilika ghafla,” amesema Malewo.
Ameeleza kuwa kuna watu waliopata msongo wa mawazo na huzuni, hawawezi kuwa salama kutokana na hali hiyo, hivyo kila mmoja anapaswa kuzungumza na watu tofauti kwa kutafakari namna ya kuanza maisha mapya na kuachana na yaliyopita ili kila mmoja awe na uwezo wa kusonga mbele kwa kasi bila kukwamishwa na matukio ya hapo awali.
SOMA: Mikakati 5 ya serikali kukabili afya ya akili
“Mtu ambaye hakupitia changamoto yoyote hawezi kutambua maumivu ya wale walikumbwa na matatizo katika vurugu hizo, sasa kila mmoja wetu anapaswa kuvaa kiatu cha mwingine na kubebea tatizo lake kwa ajili ya kujua namna ya kusaidiana ili wasahau yaliyowakumba,” amesema.
Ametoa wito kwa wadau wa saikolojia na serikali kuchukulia uzito suala hilo ili watu wapate msaada na waepuke
magonjwa wanayoweza kuwapata kutokana na kuwa na hofu.
Malewo aliishauri serikali kuweka mikakati ya wananchi kupatiwa elimu ya saikolojia mara kwa mara na kufanya tathmini ya watu walioathirika kisaikolojia kutokana na vurugu hizo ili wapatiwe msaada kabla hawajapata madhara makubwa zaidi ambayo yanaweza kuwasababishia magonjwa.
“Ni muhimu watu kujengewa uwezo wa kujiimarisha kabla hayo mambo hayajatokea, wapewe elimu ya udhibiti wa msongo wa mawazo na kukabiliana na majanga ya dharura ili waweze kukabiliana na kumudu hali zote, kukabiliana na hisia na kujenga ujasiri wakati wote,” amesema.
Ametoa wito kwa viongozi wa serikali na Watanzania kuacha matumizi ya kauli za maudhi pamoja na kutopuuzia kauli zinazotolewa na watu.
Naye mwanasaikolojia, John Ambrose amewashauri Watanzania kuepuka kutumiana ujumbe na taarifa za vitisho na matukio yaliyotokea hapo awali kwa sababu wanaweza kusababisha hofu zaidi inayoweza kuwasababishia magonjwa yanayotokana na matatizo ya ubongo.
“Kila mmoja meathirika kwa namna ya tofauti, sasa inatakiwa watu wajipatie msaada kwanza wao wenyewe kwa kujipa tafsiri nzuri kwamba tatizo lililotokea limekwisha na wasijifungie ndani, watembee ili waone maisha yamerudi kama hapo awali na waonane wa watu wengine kwa ajili ya kubadilishana mawazo,” amesema Ambrose.
Ameeleza ni vyema jamii ikaongeza ushirikiano zaidi kimawazo, kiuchumi na kijamii kwa kuwa tatizo hilo halikuwa na maandalizi, hakuna mtu aliyejiandaa na wapo waliokuwa hawana uwezo wa kupata mahitaji muhimu ikiwemo chakula.
“Kitendo cha watu kukaa ndani kimewaathiri baadhi ya watu kibishara, ndoto na mipango ya watu kwa sababu
baadhi yao hutumia mitandao kufanya shughuli zao za uchumi, kupata furaha na kuondoa upweke,” amesema.



