MKOA wa kimadini wa Geita umefanikiwa kutoa jumla ya leseni za uchimbaji mdogo wa madini 355 kwa vikundi mbalimbali vya wanawake ndani ya kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Ofisa Madini Mkazi mkoa wa kimadini Geita, Samwel Shoo amesema hayo katika semina kwa Chama cha Wachimbaji Wanawake Nchini (TAWOMA) iliyoandaliwa na kiwanda cha kusafisha madini cha Geita (GGR).
Amesema tangu mwaka 2021 hadi 2025 kina mama wameonyesha ushiriki mkubwa kwenye sekta ya madini kuanzia kwenye uchimbaji, uchenjuaji, usafishaji, uchakataji pamoja na biashara za madini.
Ameongeza pia kwa sasa kuna mitambo minne ya kuchakata dhahabu na mitambo 13 ya kuchenjua madini inayomilikiwa na wanawake huku wapo wanawake wawili wamesajiliwa kufanya biashara za madini moja kwa moja.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema serikali inaendelea kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo hasa wanawake ambapo mwaka huu mkoa wa kimadini wa Mbogwe umetangaza kutoa leseni 2,300 katika pori la Kigosi.
Amesema mbali na leseni hizo mkoa wa kimadini wa Mbogwe umepokea maombi 4,100 ambapo mchakato unafanyika kuhakikisha waombaji wenye sifa wanapata.
“Tunaenda kwenye kamati kuu, tukakulibaliane angalau kila mmoja asizidi leseni tatu hadi nne ili kila mmoja angalau apate leseni”, amesema Shigella.
“Lile eneo ambalo tulitangaza lilikuwa kama theluthi moja ya eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo kwa hiyo zipo leseni zingine kama 4,000 zinatarajiwa kutangazwa,” amesema. Shigella.
Meneja wa Benki ya Azania Tawi la Geita, Rhoda Baluya amesema watatumia fursa ya leseni mpya katika pori la akiba la Kigosi kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wachimbaji wadogo wanawake kuiunga mkono serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa GGR, Sarah Masasi amekiri mazingira rafiki ya uwekezaji kwenye sekta ya madini yaliyowekwa na serikali yamefungua milango kwa wawekezaji akiwemo yeye kujikwamua kiuchumi.
Meneja wa Idara ya Huduma za Kiuwakala wa Serikali Kutoka BoT, Sadiki Nyanzowa amewahakikishia Tawoma na Benki zingine kuwa itatoa udhamini kwa vikundi vya wanawake vitakavhotoa mikopo.