Waomba sheria ya VAT Service Levy zifumuliwe

WAFANYABIASHARA mkoani Geita wameiomba serikali kuzifanyia mapitio sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) pamoja na Sheria ya Ushuru wa Huduma (Service levy) ili wajiendeshe kwa faida.
Wafanyabiashara hao wametoa maoni yao wakati wa kikao maalumu cha kutoa maoni ya mabadilikio ya sheria ya mlipakodi yanayoratibiwa na tume maalum iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Meneja wa Kodi GGML, Godvictor Lymo amesema sheria ya VAT imekuwa ikiwaumiza zaidi wakandarasi wanaofanya kazi na taasisi za umma kwani tozo ya VAT huongezeka kadri malipo yanavyochelewa.

Amesema mbali na kuwa wafanyabiashara wanaopata kandarasi ya kutoa huduma ama kufanya kazi na taasisi za umma wamekuwa wakicheleweshewa malipo lakini sheria ya VAT haitoi msamaha kwa hilo.
“Sasa yule mkandarasi anaadhibiwa kwa kushindwa kulipa VAT ambayo alitakiwa aikusanye kutoka kwa mteja wake ambaye ni taasisi ya serikali kwenda kwa mamlaka ya mapato.
“Lakini kwa sababu hajalipwa anashindwa kuikusanya matokeo yake, hata anapokuja kulipwa yale madeni yanakuwa ni makubwa na kupelekea kupata hasara, amesema Lyimo.

Lyimo amesema sheria hiyo ya VAT imesababaisha baadhi yawakanadarasi kupoteza mitaji na hata kushindwa kuendelea na biashara zao hali ambayo imeipunguzia serikali uwigo wa walipa kodi.
Ameshauri mabadiliko yafanyike kuendana sheria ya VAT visiwani Zanzibar ambayo haitoi adhabu ya malimbikizo ya tozo kwa mkandarasi anayefanya kazi na serikali iwapo atachelea kulipa VAT.
Mmiliki wa nyumba za kulala wageni na duka la dawa, Masumbuko Wazaeli amesema ni vyema ushuru wa huduma kwa mteja (Service Levy) uondolewe kwani unaongeza mzigo kwa walipa kodi wadogo.
“Mapendekezo yangu kwenye kodi hiyo, wasubiri halmashauri hesabu zifanywe ionekane kwa mwaka ameingiza shilingi ngapi, gharama zake ni ngapi, faida inayobaki ndio itolewe asilimia 10”, amesema.
Amesema miaka ya hivi karibuni serikali iliondoa services levy kwa wamiliki wa vibanda na maduka madogo lakini wameshitushwa na hivi karibuni kuanza kupokea barua zikiwataka walipe deni la service levy.
Ameiomba serikali pia kuondoa sheria inayomtaka mfanyabishara aliyeingia kwenye mzunguko wa mauzo ya Sh milioni 100 kwa mwaka kuingizwa kwenye VAT.
Mwenyekiti wa Tume ya Maboresho ya Kodi nchini, Balozi Ombeni Sefue amekiri kupokea maoni, mapendekezo na ushauri wa wafanyabaiashara hao na kuahidi kufanyia kazi kwa maslahi ya taifa.



