‘Wapiga kura Uganda wanazingatia sifa za mgombea’

MSEMAJI wa chama tawala cha Uganda, National Resistance Movement (NRM), amesema kuwa wapiga kura wa nchi hiyo wako tayari kumuunga mkono mgombea wa urais kutoka katika mazingira yoyote, mradi awe na sifa zinazokubalika za uongozi.
Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), msemaji wa NRM, Emmanuel Lumala Dombo, amesema kuwa historia ya mgombea, iwe ya kiraia au kijeshi, si kigezo cha msingi kinachoamua uamuzi wa wapiga kura wa Uganda.
Amesema kuwa iwapo wapiga kura wangekuwa wanazingatia historia ya kijeshi pekee, basi wagombea waliowahi kuwa wanajeshi wangekuwa wakipata uungwaji mkono mkubwa mara zote katika chaguzi zilizopita. Dombo alitolea mfano mwanasiasa wa upinzani, Dk. Kizza Besigye, aliyewahi kuwania urais mara kadhaa dhidi ya Rais Yoweri Museveni.
“Wakati Dk. Besigye alipojitokeza kuwania urais dhidi ya Rais Museveni, kulikuwa na dhana kuwa angekuwa mgombea bora kutokana na historia yake ya kijeshi. Hata hivyo, alishiriki uchaguzi lakini hakufanikiwa kushinda,” alisema. SOMA: Museveni aidhinishwa kugombea urais
Kwa mujibu wa Dombo, katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Januari 15, mmoja wa wagombea wanaotajwa kutoa ushindani mkubwa ni mwanamuziki aliyegeuka mwanasiasa, Robert Kyagulanyi, maarufu kwa jina la kisanii Bobi Wine.
Akizungumzia uvumi unaodai kuwa Rais Museveni anamuandaa mwanawe, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kama mrithi wake wa kisiasa, Dombo alisema chama cha NRM kina taratibu za wazi za ndani kuhusu uongozi na uteuzi wa wagombea.
Amesema kuwa endapo Jenerali Muhoozi ataamua kuwania wadhifa wa kisiasa kupitia NRM, atalazimika kufuata taratibu zote za chama hicho kama wanachama wengine. “Ikiwa ataamua kutumia uzoefu wake wa kijeshi kama sehemu ya wasifu wake wa uongozi, bado atalazimika kuthibitisha sifa nyingine muhimu zinazohitajika ili kuaminiwa na wapiga kura,” alisema Dombo. Wananchi wa Uganda wanatarajiwa kupiga kura Januari 15 kumchagua Rais na wabunge wa Bunge la Taifa.



