MADAKTARI wa wanyama Tanzania wameshauriwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanatokomeza magonjwa ya wanyama kuongeza tija biashara ya nyama kwenye soko la kimataifa na serikali kuongeza mapato.
Mwenyekiti wa Chama Cha Kitaaluma cha Wanyama Tanzania (TVA), Profesa Esron Karimuribo ametoa wito huo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Arusha leo Desemba 2, 2024.
Amesema kuanzia kesho kutakuwa na Kongamano la 42 la siku tatu linalotarajiwa kufunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Prof. Esron Karimuribo amesema katika mwaka 1970 hadi mwaka 1980 mifugo ilikuwa ikikabiliwa na magonjwa mengi, lakini hali hiyo imebadilika na magonjwa yote ya kuambukiza yametokomezwa kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na madaktari wa mifugo.
Amesema TVA imekuwa ikishirikiana na serikali katika kukabiliana na magonjwa ya wanyama na kufikia hatua mifugo kukubalika kuuzwa nje ya nchi na kuingizia serikali fedha za kigeni.
Aidha, mwenyekiti huyo ameishukuru serikali kwa kuongeza bajeti Wizara ya Mifugo na Uvuvi hadi kufikia Sh bilioni 460 na hiyo inawapa nguvu wataalamu kufanya kazi katika mazingira mazuri na kusonga mbele.
Prof Karimuribo ambaye ni Mhadhiri Chuo Kikuu Cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro amesema serikali imetenga Sh bilioni 28 kwa ajili ya chanjo ya mifugo hiyo imewapa moyo na nguvu wataalamu wa mifugo kuona kuwa idara hiyo inapewa kipaumbele katika kuhakikisha magonjwa ya mifugo na ya mlipuko yanathibitiwa kwa maslahi ya nchi na sio vinginevyo.
Naye Katibu Msaidizi wa TVA na mwakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Caroline Uronu amesema kuwa chama hicho ni mmoja ya vyama vya kitaalamu vikongwe nchini na kinatambulika serikalini na kinaisaidia sana serikali hususani Wizara Mifugo na Uvuvi katika kupambana na magonjwa ya mifugo na kuthibiti magonjwa ya milipuko.
Mhadhiri kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela , Profesa Gabriel Shirima amesema kuwa ubora wa mifugo na wanyama kwa ujumla wakiwa salama na afya ya binadamu inakuwa salama na uwezekano wa ongezeko la mifugo na wanyama ikawa kubwa na nchi kuongeza mapato.
Kongamo hilo linatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 2000 wa hapa nchini na wataalamu kutoka Jumuiya ya Madola wamealikwa katika kongamano hilo lengo ni kutaka kuhakikisha Tanzania na Afrika inakuwa na wanyama wenye ubora ambapo kwa upande wa mifugo itaongeza soko la kimataifa