Wasimamizi uchaguzi watakiwa kusimamia viapo

SHINYANGA: WASIMAMIZI wa uchaguzi 83 kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu wametakiwa kusimamia viapo vyao na kujitoa kwenye chama chochote cha Kisiasa kwenye kipindi hiki cha uchaguzi ili kuepuka migogoro.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ( INEC) Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mh Jaji Jacobs Mwambegele amesema leo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu yaliyoanza tarehe 21 hadi 23 kwa waratibu,wasimamizi na wasimamizi wasaidizi .
Jaji Mwambegele amewaomba wasimamie viapo vyao vya kutunza siri na kutokuwa wanachama wa chama chochote cha siasa katika kipindi chote cha uchaguzi na kutekeleza vizuri majukumu yao.
“Tume iliwaridhia maafisa uchaguzi na maafisa ununuzi kutekeleza kazi za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambapo uteuzi wenu umezingatia masharti ya kifungu cha sita(1),(2) na 5 na kifungu cha nane ( 1) na( 2) vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani,” amesema Mwambegele.

Jaji Mwambegele amewasihi wajiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko utoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi pia wahakikishe wanazingatia ipasavyo katiba ,shera,kanuni ,miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na tume.
Jaji Mwambegele amesema vyama vyote vya siasa vilivyo na usajili vishirikishwe kwa ukamilifu kwa hatua zote kwa kuzingatia matakwa ya katika, sheria, kanuni na maelekezo.
Jaji Mwambegele amesema ajira za watendaji wa vituo zizingatie kuajiri watendaji wenye weledi wanaojitambua,wazalendo,waadilifu na wachapakazi na kucha upendeleo kwa kuajiri ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.
Jaji Mwambegele amesema katika mafunzo hayo watajifunza mada 12 pamoja na mambo mengine na kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na kujadiliana namna ya kufanikisha uchaguzi katika maeneo yenu.



