Wasira aongoza kampeni Kalenga

IRINGA: Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, ameongoza uzinduzi wa kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Kalenga, Iringa na kuwataka wananchi “kuipa CCM ridhaa ya kishindo” ili iendelee kusukuma gurudumu la maendeleo.

Katika mkutano uliofurika mamia ya wananchi, viongozi wa chama na wazee wa mila katika Kijiji cha Kidamali, Kata ya Nzihi, Wasira alimkabidhi mgombea ubunge Jackson Kiswaga Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya kitaifa na ile ya Mkoa wa Iringa, akisisitiza:

“CCM ni chama chenye historia ya kuahidi na kutekeleza. Tulisema tutaboresha huduma za maji, afya, elimu na zinginezo—na tumefanya. Huu ni ushahidi wa chama kinachoweza kuomba tena kura kwa uhalali.

Wasira alifafanua kuwa katika Ilani mpya ya 2025–2030, Kalenga itapata shule tano za msingi na sekondari, zahanati mbili na vituo vya afya vitatu, pamoja na kuendeleza miradi ya barabara, ikiwemo barabara ya kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa lengo la kufungua fursa za utalii na ajira kwa vijana.

Alisisitiza kuwa kilimo na ufugaji vitabaki kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Kalenga, akiahidi vituo vya zana za kilimo na ruzuku za pembejeo ili kuruhusu wakulima kulima msimu wa kiangazi na mvua, sambamba na uwekezaji katika umwagiliaji na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.

“Kilimo hakiwezi kuachwa mikononi mwa mvua pekee. Tutawapa wakulima mikopo ya zana za kilimo na kuhakikisha mbolea inafika kwa wakati. Hii ndiyo CCM ya vitendo,” alisema.

Kiswaga, anayewania ubunge kwa muhula wa pili, alishangiliwa na wazee wa mila na viongozi wa chama waliompongeza kwa “uongozi wa matokeo.”

“Kalenga ni ngome ya CCM. Oktoba 29, tutamvisha mama Samia kura 99.9%, mimi 99.8% na madiwani 99.7%. Tutazunguka nyumba kwa nyumba kuhakikisha ushindi wa kishindo,” aliahidi Kiswaga kwa shangwe za umati.

Aliyekuwa Mbunge wa Isimani William Lukuvi alisisitiza umuhimu wa kuendeleza uongozi wa muda mrefu wenye uzoefu, akitoa mfano wa mafanikio aliyoyapata Isimani chini ya uongozi wake.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Salim Abri “Asas” aliahidi kura za “bila kuyumba” kwa chama hicho, huku Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Daud Yassin akiorodhesha miradi mikubwa ya awamu ya sita katika maji, nishati, barabara na afya kama ushahidi wa utekelezaji wa Ilani.

Kwa kauli moja, viongozi hao walisisitiza kuwa CCM si chama cha maneno bali cha matendo, wakiahidi kuendelea kudumisha amani, mshikamano na maendeleo kwa wananchi wa Kalenga na mkoa mzima wa Iringa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button