Wachambuzi watoa ‘tano’ kampeni za kistaarabu

PWANI : JESHI la Polisi, wachambuzi na wasomi nchini wamepongeza vyama vya siasa kwa kufanya kampeni zilizojaa amani, utulivu na zinazohimiza mshikamano kwa Watanzania katika kipindi cha mwezi mmoja tangu kuanza kwa kampeni hizo.

Sambamba na hilo, wamekumbusha vyama vya siasa kutembea kwenye Ilani yao kwenye majukwaa ya kuomba kura na viepuke kutoa ahadi zisizotekelezeka. Wachambuzi wa masuala ya siasa na Jeshi la Polisi walitoa pongezi hizo jana walipozungumza na HabariLEO kuhusu mwenendo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu na tathmini ya mwezi mmoja tangu zizinduliwe Agosti 28.

Hakuna udhalilishaji Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dk Rose Reuben alisema hakuna udhalilishaji uliofanywa na vyombo vya habari katika kipindi cha mwezi mmoja wa kampeni. Alisema kasoro iliyojitokeza ni kwa wananchi wanaotoa maoni mitandaoni kuhusu wagombea na kushauri mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua watu hao wanaotoa maoni yanayodhalilisha na kutweza utu wa mtu.

Polisi na usalama Jeshi la Polisi nchini limesema katika kipindi cha mwezi mmoja wa kampeni uliopita hali ya usalama nchini ilikuwa shwari. Msemaji wa jeshi hilo, David Misime alisema hali hiyo imechangiwa na wagombea, vyama vya siasa, wananchi na wakereketwa kufuata sheria kikamilifu.

Aliongeza kuwa wagombea wamejitahidi kufuata ratiba iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) pamoja na kumaliza mikutano yao kwa wakati. “Tatizo kidogo lililojitokeza katika baadhi ya maeneo kuna watu wanabandua na kuchana mabango ya wagombea.

Hawa wamekamatwa na wanachukuliwa hatua za kisheria kukomesha hali hiyo,” aliongeza Kamanda Misime. Vyama vitembee kwenye ilani Wachambuzi wamepongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutembea kwenye Ilani yake wakati wa kumnadi mgombea wake na kushauri vyama vya upinzani kurudi kwenye Ilani za vyama vyao wakati wa kunadi wagombea wao. SOMA: Chaumma kuteua wagombea urais leo

Mhadhiri wa Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo alisema tangu siku ya kwanza CCM imekuwa ikitoa ahadi zake kwa wananchi kutokana na matakwa ya Ilani yake hali inayofanya ahadi zake kuwa zinazotekelezeka. Alisema ahadi za wagombea wote siku zote zinatakiwa kuwa za kutekelezeka na zinazoeleza changamoto za wananchi na namna bora ya kuzitatua ili kuleta unafuu wa kimaisha kwa wananchi.

Profesa Kinyondo alisema tofauti na ahadi za CCM, vyama vya upinzani vimekuwa vikitoa ahadi zisizotekelezeka kitu ambacho kinatoa nafasi kubwa kwa CCM kuvishinda katika uwasilishaji wa majawabu ya shida za wananchi. “Ahadi za vyama vya upinzani si matokeo ya Ilani zao, ni lolote linalomtoka mdomoni,” alisema Profesa Kinyondo na kuvishauri vyama vya upinzani vijitahidi kuifanya ngwe ya pili ya kampeni kuwa na maana.

Sambamba na hilo, Profesa Kinyondo aliwashauri wagombea wa upinzani na vyama vyao kujaribu kukutana na kutengeneza mpango mkakati wa namna ya kuzitumia siku 30 zilizobaki ili wawatendee haki Watanzania.

Alisema ni jambo jema kuona baadhi ya vyama kikiwemo CCM kuahidi mabadiliko ya Katiba. Naye Mchambuzi wa Masuala ya Kilimo, Philipo Mrutu alisema katika kipindi cha mwezi mmoja wa kampeni Watanzania wameshuhudia na kusikia ahadi za chama tawala na Ilani yake mkononi na vyama vya upinzani bila Ilani yao mkononi.

“Katika kipindi chote cha mwezi mzima tumeshuhudia ahadi zinazotekelezeka kutoka CCM na ahadi zisizotekelezeka kutoka vyama vya upinzani. Chama tawala kinatembea kwenye Ilani yake wakati upinzani wanatoa ahadi bila kuangalia Ilani yao inataka nini,” aliongeza Mrutu.

Ahadi zisizotekelezeka, zilizotawala Mrutu ambaye pia ni mtaalamu wa kilimo alisema vyama vya upinzani vinatoa ahadi zisizozingatia mahitaji ya wananchi akitolea mfano wa chama kimojawapo kilichoahidi kumbakisha Samia Ikulu endapo kitapata ridhaa ya kuongoza taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button