Wataalam Agota, ISGE kukutana Zanzibar

ZANZIBAR; WATAALAMU kutoka Shirika la Kimataifa la Upasuaji wa Wanawake (ISGE) na Chama cha Wanagyna na Wakunga Tanzania (AGOTA) wanatarajia kukutana Zanzibar Mei 21-24, 2025.

Taarifa iliyotolewa na Meneja wa mkutano huo, Ibrahim Mitawi wa Showtime Company leo Novemba 25, 2024 imeeleza huo utakuwa mkutano wa 7 wa ISGE, pamoja na kongamano la kitaifa la 28 la AGOTA.

“Kama Meneja wa mkutano huu, ninawakaribisha washiriki wote Zanzibar, eneo bora la Tanzania kwa mikutano na matukio,” amesema Mitawi.

Advertisement

Kwa upande wake Rais wa AGOTA, Dk Batilda Ngarina, ameeleza kuwa mada ya mwaka huu itakuwa ‘Taaluma ya Upasuaji wa Tundu Dogo kwa Wanawake kwa Mgonjwa Sahihi katika Muktadha Sahihi Barani Afrika.’

“Tukio hili muhimu linakusudia kukuza ushirikiano na kubadilishana maarifa kati ya wataalamu wa gainakoloji, watafiti, na viongozi wa sekta. Mada inasisitiza umuhimu wa njia za upasuaji zilizobinafsishwa katika kuboresha huduma za afya za wanawake kote Afrika,” amesema Dk Ngarina.

Amesema mkutano huo ni fursa nzuri kwa wataalamu kuungana, kupata uzoefu, na kujenga ushirikiano mpya ambao utaweza kuleta mabadiliko chanya katika huduma za afya za wanawake barani Afrika.

“Watakaokuwepo watashiriki katika mpango kamambe unaojumuisha warsha, vikao vya mafunzo, na mawasilisho ya wataalamu yanayochangia maendeleo katika Taaluma ya Upasuaji wa Tundu Dogo kwa Wanawake (MIGS).

“Tunaalika wataalamu wote katika uwanja wa gynaecology na obstetrics kujiunga nasi ili kujiimarisha. Maoni na michango yenu ni ya thamani katika kuendeleza uwanja wa upasuaji wa gynecologic,” amesema Dk Hassanat wa AGOTA.