Watanzania kupewa kipaumbele sekta ya madini

MWANZA: SERIKALI kupitia Tume ya Madini itaendelea kusimamia manunuzi ya bidhaa na huduma kwa kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa watanzania kwa mujibu wa Sheria ya Madini,Sura ya 123.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde jijini Mwanza  akifungua kiwanda cha ukarabati wa mitambo ya uchimbaji na uchorongaji kinachoendeshwa chini ya ubia wa Kampuni ya SANDVIK ya Sweden na JC GEARS GROUP LTD cha Tanzania.

Advertisement

Mavunde amesema, kazi kubwa imefanywa na serikali chini ya uongozi wa Rais, Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kunakuwa na   mazingira mazuri ya uwekezaji na hivyo kuvutia ushiriki wa kampuni kubwa za madini katika mnyororo mzima wa thamani kwenye sekta ya madini.

“Kwa kuzingatia hilo serikali ilifanya mabadiliko kwenye sheria ya madini mwaka 2017 yaliyopelekea kutungwa kwa kanuni za ushirikishaji wa watanzania za mwaka 2018 ili kuweka usimamizi thabiti ya ushiriki wa watanzania kwenye sekta ya madini, ” amesema Mavunde na kuongeza

” Matunda ya kanuni ni hapa leo kwenye ufunguzi wa kiwanda cha kukarabati mitambo ya huduma za madini ambacho kinamilikiwa kwa ubia kati ya kampuni ya kitanzania na ya Sweden, ” amesema.

Amesema huo ndio muelekeo ambao serikali itauchukua kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanashiriki katika sekta ya madini.

“Miaka michache iliyopita huduma na bidhaa migodini zilikuwa zinapatikana nje ya nchi kwa asilimia zaidi ya 90, kwasasa tunaendelea kuwajengea uwezo watanzania ili haya yote yafanyike ndani ya nchi kwa asilimia kubwa,” amesema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JC GEARS GROUP LTD, James Makanyaga alisema  mabadiliko ya sheria ya madini yameongeza ushiriki wa watanzania kwenye uchumi wa sekta ya madini kwa kiwango kikubwa na pia yamechochea upatikanaji wa ajira kwa  watanzania.