Watanzania kuwekeza sarafu na iDollar Fund

DAR ES SALAAM: MFUKO wa Uwekezaji wa Pamoja iDollar Fund utawezesha Watanzania kuwekeza sarafu za kigeni kama vile Dola, Pauni na sarafu nyingine za mataifa mbalimbali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama anasema.

Hatua hiyo ni juhudi za kuimarisha uwekezaji nchini na kuongeza mchango wa fedha za kigeni kwa uchumi wa taifa ambapo Kampuni ya iTrust Finance Limited imezindua rasmi mfuko huo.

CPA Nicodemus Mkama amesema hatua hiyo ni matokeo ya mazingira bora ya kisera na kisheria yaliyowekwa na serikali kupitia CMSA ili kuwezesha maendeleo ya sekta ya masoko ya mitaji.

“Mfuko huu ni nyenzo muhimu kwa ukusanyaji wa fedha za kigeni. Unachangia katika uthabiti wa uchumi na kuimarisha uwezo wa nchi kushughulikia changamoto za kigeni. Pia, mfuko huu utawawezesha Watanzania kuwekeza fedha walizonazo katika akaunti zao za sarafu za kigeni,” amesema CPA Mkama.

Ameongeza kuwa kwa kuzinduliwa kwa mfuko huu, Tanzania sasa inaungana na nchi nyingine Afrika ambazo tayari zimeanzisha mifumo kama hii, ikiwemo Kenya, Afrika Kusini, Mauritius na Ghana, pia amewahimiza Watanzania, taasisi na makampuni mbalimbali kuchangamkia fursa hii ili kuongeza uwekezaji wao kwa kutumia fedha za kigeni.

Aidha, CPA Mkama ameeleza kuwa iDollar ni sehemu ya mifuko ya uwekezaji iliyosajiliwa na kuidhinishwa na CMSA, pamoja na ile inayoendeshwa na kampuni ya UTT AMIS.

SOMA ZAIDI: Majaliwa: Tanzania ni mahali sahihi kuwekeza

Alibainisha kuwa mfuko huo pia utatoa fursa kwa Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) kuwekeza fedha zao na kusaidia kukuza uchumi wa ndani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa iTrust Finance Limited, Profesa Mohamed Warsame, amesema mfuko wa iDollar umelenga kutoa suluhisho kwa Watanzania wengi ambao tayari wana akaunti za dola kwenye benki, lakini hukosa njia rasmi na faida kubwa za kuwekeza fedha hizo.

“Mfuko huu unatoa fursa kwa Mtanzania kuwekeza akiwa na dola kwenye akaunti yake, na pia kupata faida zake kwa dola. Tumelazimika kuja na suluhisho hili kutokana na mabadiliko ya sheria ya nchi, ambapo sasa dola haziruhusiwi kutumika moja kwa moja katika miamala ya ndani kama vile malipo ya kodi, ada au upangishaji wa nyumba,” amesema Prof. Warsame.

Amesema kutokana na hatua hiyo ya kisheria, benki kuu ya Tanzania imeelekeza Watanzania kutotumia fedha za kigeni katika miamala ya ndani, hivyo mfuko huu unakuja kama njia mbadala ya kuzitumia fedha hizo kwa uwekezaji wenye tija na manufaa.

Mfuko wa iDollar utasimamiwa na kampuni ya iTrust Finance Limited, ambayo ina leseni kutoka CMSA, huku usimamizi wa fedha ukifanyika kupitia Benki ya CRDB.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button