Watanzania waepuke mambo yasiyo ya kiungwana wakati wa kampeni

LEO Agosti 28, 2025 ndiyo siku rasmi ambayo kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, zinaanza. Kipindi cha kampeni ni kipindi ambacho joto la siasa linakuwa juu kuliko wakati mwingine wowote na hasa kadiri siku zinavyoenda kuikaribia siku ya uchaguzi.

Kila mwaka wa uchaguzi katika historia ya nchi, huwa na aina yake ya namna kampeni zinavyoenda kutegemea na mwenendo wa kisiasa katika mwaka husika. Mwenendo wa kisiasa huamuliwa na aina ya wagombea, hali ya vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi na hata namna wananchi wanavyoitikia katika mchakato mzima wa uchaguzi katika mwaka husika. SOMA: Tusikilize sera kwenye kampeni, wavuruga amani tuwakatae

Wakati wa kampeni ni wakati ambao upo uwezekano wa kutokea vurugu au vitendo vingine vyovyote visivyokuwa vya kiungwana kama umakini usipokuwepo. Yapo mambo mengi ambayo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), viongozi mbalimbali na hata asasi mbalimbali zimekuwa zikitumia muda wake kutoa tahadhari kuhakikisha wagombea pamoja na wananchi kuyaepuka katika kipindi cha uchaguzi hasa wakati wa kampeni kuhakikisha hakuna athari hasi yanatokea katika wakati huo.

Baadhi ya mambo ambayo yanasisitizwa kuyaepuka ni pamoja na vurugu, kauli za chuki, ghasia na kauli zenye kulenga kuwagawa wananchi. Kadhalika, vyombo vya habari vikiwa ni kiungo muhimu katika kuhakikisha Uchaguzi Mkuu katika nchi yoyote unakwenda vizuri na kwa amani, vimehadharishwa vya kutosha kuhusiana na kuepuka mambo yanayoweza kusababisha vurugu.

Akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari kuelekea Uchaguzi Mkuu, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima alisema: “Tunatarajia hamtasambaza maudhui yanayoweza kuchochea ghasia, mgawanyiko au lugha za chuki.”

Kailima alisisitiza matarajio ya INEC kwa vyombo vya habari ni kuripoti matukio yanayohusiana na uchaguzi kwa wakati, akasisitiza: “Natumaini mtatumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa rasmi na zilizothibitishwa kuhusu uchaguzi na kutoa nafasi kwa tume kujibu tuhuma au malalamiko yanayoelekezwa kwake”.

Wananchi pia wamekuwa wakikumbushwa mara kwa mara jukumu lao katika kuilinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi ambapo muda wa kampeni ndio muda hasa wanapaswa kukumbuka jukumu hilo. Jambo kubwa ambalo wamekuwa wakikumbushwa ni kutokukubali rushwa ambayo ni adui mkubwa katika mchakato mzima wa uchaguzi na kwamba wagombea wanaotoa rushwa ili wachaguliwe si viongozi sahihi

Hivyo, kampeni zinapoanza leo, ni muhimu Watanzania kuepuka mambo yote yasiyo ya kiungwana na yanayokwenda kinyume na utaratibu ambayo pia yanaweza kuvunja amani na kusababisha kampeni kutokwenda kama zinavyopaswa kuwa.

Vyama vya siasa, wagombea na wananchi wote wanapaswa kujua kipindi cha kampeni ni cha kusikiliza sera, ahadi za wagombea na vyama, ni kipindi cha kuchambua ilani za vyama na kuona chama kipi kinaweza kuivusha nchi katika maendeleo na si vinginevyo. Tanzania inahitaji amani leo, kesho, keshokutwa na mtondogoo hivyo ni muhimu kampeni zizingatie kulinda amani na kujenga taifa lenye umoja na mshikamano.

Habari Zifananazo

4 Comments

  1. I just got paid $22k working off my laptop this month!** And if you think that’s cool, my divorced friend has twin toddlers and made over $22620 her first month. details on this website**Want the secret?** Copy this Website and choose HOME TECH OR MEDIA…..

    Here is I started_______ https://Www.CashHive1.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button