Watendaji INEC wafundwa maadili mikoa ya Kusini

MTWARA: TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka watendaji wa uchaguzi katika mikoa wa Mtwara na Lindi kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za tume hiyo kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Akizungumza jana wakati wa mafunzo ya siku tatu yanayoendelea mkoani Mtwara kwa watendaji hao wa uchaguzi katika hiyo, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchagu, Balozi Omar Mapuri amesema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali kikatiba na kisheria ambazo zinapaswa kufatwa na kuzingatiwa.

‘’Hatua na taratibu hizi ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri na wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi,”amesema Mapuri.
Mafunzo hayo yamekutanisha watendaji mbalimbali kwenye mikoa hiyo wakiwemo waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, yaliyofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwaasa watendaji hao kuwa, pamoja na uzoefu ambao baadhi yao wanao katika uendeshaji wa uchaguzi lakini wasiache kusoma katiba, sheria, kanuni, taratibu, miongozo lakini wafate na watekeleze maelekezo mbalimbali yatakayokuwa yanatolewa na tume hiyo.

‘’Someni kwa umakini katiba, sheria, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotelewa na yakatayotolewa na tume na ulizeni ili mpate kufafanuliwa kwenye maeneo ambayo kwa namna moja au nyingine pengine yatakuwa na changamoto za kufahamu ili kuwarasishia katika utekelezaji wenu wa kazi za uchaguzi,” amesisitiza Mapuri
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura wa INEC Giveness Aswile amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo na uelewa zaidi watendaji hao wa kusimamia shughuli hizo za uchaguzi.



