Watoto waende shule – DC Tandahimba

MADIWANI katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara wametakiwa kuendelea kuwahimiza wazazi na walezi ambao bado hawajawapeleka watoto shule wawapeleke ili wakapate masomo na kuhakikisha chakula kinapatikana shuleni.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Francis Mkuti amesema kama kuna baadhi ya mzazi au mlezi ambaye mpaka sasa bado hajampeleka mtoto shule kipindi zipofunguliwa Januari 13, 2025 ajitahidi katika hilo na kila diwani kwenye eneo lake ahakikishe analisimamia kikamilifu zoezi hilo.

Hayo yamejiri wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kuhusu kuwasilisha taarifa mbalimbali za maendeleo ya kata robo ya pili mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika kwenye halmashauri hiyo.

Advertisement

Aidha serikali inaendelea kuhakikisha miundombinu ya kusomea inakuwa mizuri kwa kuwekeza fedha nyingi kwenye sekta hiyo ili vijana wao wasome katika mazingira mazuri ili wapate ufaulu mzuri.

Pia ametumia nafasi hiyo kutilia mkazo suala hilo wazazi na walezi kuchangia chakula shuleni kwasababu ni muhimu kwani mtoto akila akashiba anakuwa na usikivu mzuri darasani.

Hata hivyo amesisitiza kutumia mvua zinazonyesha kulima mazao ya chakula, ukusanyaji wa mapato, utunzaji wa mazingira pamoja na kuendelea kuimarisha suala la ulinzi na usalama kwenye maeneo yao.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Baisa Baisa amewaomba madiwani hao kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kwenye maeneo yao ili iweze kukamilika na kutumika kwa wakati.

“Miradi inapokuja kwenye kata yako jukumu la diwani ni kuhakikisha anausimamia mradi huo ukamilike ili wananchi wa eneo lako wafaidike nao lakini mradi unapokamilika kwa wakati maendeleo yanazidi kupatikana kwenye maeneo yetu na kukuza uchumi wa wananchi na mapato ya halmashauri kwa ujumla “amesema Baisa

Mbali na hilo madiwani hao wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia bei ya korosho katika msimu wa kilimo mwaka 2024/2025 ambayo imeuzwa kwa bei ya juu ikilinganishwa na misimu iliyopita huko nyuma.

Katika hatua nyingine mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Edith Shayo ametoa wito kwa madiwani hao kuwasistiza wananchi wilayani humo kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.