Watoto wenye ulemavu kupewa viti mwendo

ARUSHA: SHIRIKA la World Vision Tanzania limeeleza kuwa litasaidia utoaji wa viti mwendo kwa watoto wenye ulemavu katika kata za Naberera na Oljoro zilizopo Wilaya ya Simanjiro ili viwawezeshe kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi serikalini madawati 408 kwa shule za sekondari na msingi wilayani Simanjiro, Meneja wa Shirika la World Vision Tanzania Wilaya ya Simanjiro Samuel Charles alisema hivi sasa wameanza kuwawasiliana na viongozi wa kijiji kwa ajili ya masuala ya watu wenye ulemavu ili waweze kupatiwa msaada huo.

Ameema katika kukabidhi viti hivyo wana mpango wa kutoa vitimwendo kwa watoto zaidi ya 50 ambavyo vitawawezesha kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine

“Mkakati ni kuwa wiki ijayo tutawasiliana na wataalamu kutoka CCBRT ambao watakuja kufanya utambuzi na wataangalia huyu mtu anahitaji kipi kulingana na mazingira yake na sisi kama shirika tunashughulika na watoto chini ya miaka 17 hivyo tutatambua kila kijiji watoto wanaohitaji huo msaada na baada ya utambuzi watatoa viti 50 hadi 60 katika kata ya Naberera na Oljoro,”amesema Charles.

Aidha katika hatua nyingine World Vision Tanzania limekabidhi jumla ya madawati 408 kwa shule mbalimbali zilizopo kata ya Naberera na Oljoro wilayani Simanjiro.

Madawati hayo ni kupitia Programu ya Maendeleo Naberera ambapo madawati 150 yamekabidhiwa kwa shule mbili za msingi ambazo ni Namalulu na Landanai.

Pia Madawati 258 kwa msaada wa wafadhili kutoka Marekani (Gift in Kind) yamekabidhiwa kwa shule ya Sekondari Oljoro namba 5 ambayo ni jumla ya madawati 129, Sekondari Embris madawati 90 na Sekondari Naberera madawati 39.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Marko Masala amewashukuru Shirika la World Vision Tanzania kwa kuendelea kusaidia jamii katika miradi hiyo ya maendeleo na kusema wanaunga mkono na wataendelea kushirikiana nao katika masuala ya afya, maji na elimu kwani bado yanahitajika.

Shirika hilo linatekeleza programu mbili za maendeleo katika vijiji 11 vya kata mbili za Oljoro na Naberera ambapo mradi huo ni wa miaka 12 huku utekelezi ukifikia mwaka wa pili na shughuli zinazotekelezwa ni kuwawezesha wananchi kiuchumi ,kuboresha miundombinu ya huduma za afya na elimu, upatikanaji wa maji safi na salama,kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya ngazi ya jamii na kuhamasisha lishe bora,usafi wa mazingira pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button