Watu 23 wajeruhiwa ajali Mikindani

WATU 23 wamejeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi la Shule ya Msingi Salem kugongana na gari la Jeshi la Wananchi (JWTZ) eneo la Migomigo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.

Ajali hiyo imetokea jana majira ya saa 1 jioni (Novemba 28,2024) katika eneo hilo la migomigo barabara ya kutokea wilayani Newala mkoani humo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara ya Ligula, Zawadi Bwanali amethibitisha kuwapokea majeruhi hao 23 wa ajali hiyo ambapo kati ya hao wanafunzi ni 20, walimu wawili na dereva mmoja.

Advertisement

Amesema majeruhi wameanza kupokelewa hospitalini hapo majira ya saa 1 usiku na kuanza kupatiwa matibabu ambapo mmoja kati ya wanafunzi hao alihamishiwa hospitali ya rufaa ya kanda ya kusini mkoani humo kwa ajili ya matibabu zaidi.

‘’Niwatoe hofu wananchi wasipaniki huduma zinaendelea na wengi tumeshawafanyia uchunguzi tuliona hawana shinda tumewaruhu kurudi nyumbani,’’amesema Bwanali

Ameongeza kuwa: ‘’Hawa wengine wamepata michubuko midogo midogo na wale wengine ambao walichanika tumewashona na hali zao zitakapokuwa zimeendelea kuimarika tunawaruhusu.’’

Aidha ajili hiyo imetokea wakati wanafunzo hao alipokuwa wakitokea uwanja wa ndege mkoani humo kwa ajili ya ziara ya kimasomo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara SACP Issa Suleiman amesema ajali hiyo imehusisha basi hilo la shule ya msingi ya salem na gari la jeshi aina ya lori katika eneo hilo la migomigo kwenye manispaa hiyo na uchunguzi wa ajali hiyo bado unaendelea ili kubaini chanzo cha ajali.