Watu 33,000 hufariki matumizi nishati isiyo safi

ARUSHA: TAKRIBANI watu 33,000 kwa mwaka wanafariki nchini tanzania ikiwa ni moja ya athari ya matumizi ya nishati isiyo safi na salama.

Ofisa Nishati Mkuu kutoka Wizara ya Nishati, Mussa Abbas ameelza hayo leo Januari 11,2025 katika hafla maalumu ya uhamasishaji na kutoa elimu ya nishati safi ya kupikia kwa viongozi wa Dini ya Kiislam jijini Arusha inayofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), chini ya uratibu wa Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo.

Aidha, Mussa amesema takribani 82% ya watanzania hutegemea tungamo taka kama kuni na mkaa kwa kupikia, hali inayochangia madhara makubwa ya kiafya, kimazingira, na kijamii, huku akisisitiza umuhimu wa elimu na rasilimali ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

Advertisement

Pia ameeleza kuwa watu takriban bilioni 2.3 duniani bado hawajafanikiwa kutumia nishati safi ya kupikia huku chini Jangwa la Sahara kwa Afrika wakiwa watu milioni 990.

“Takribani watu milioni 3 dunia nzima huwa wanafariki kwa magonjwa ya hewa ambayo yanatokana na matumizi ya nishati isiyo safi, vilevile katika watu hao milioni 3, takribani 60% huwa ni wanawake na watoto, na kwa Afrika pekee takribani watu laki 4 mpaka 7 hufariki kutokana na madhara yanayosababishwa na nishati isiyo safi, na kwa Tanzania takribani watu elfu thelathini na tatu (33000) hufariki kila mwaka kutokana na matatizo hayo”, ameeleza Musa.

Ameeleza kuwa Wizara ya Nishati ina Sera ya Nishati ya mwaka 2015 ambayo imeweka bayana kwamba Tanzania inatakiwa kutoka kwenye matumizi ya kuni na mkaa kwenda kwenye matumizi ya kisasa ya kutumia nishati safi. Aidha ameeleza kuwa sera hiyo imeweka mikakati mbalimbali ya kuwezesha utekelezaji wa matumizi ya nishati safi.

Aidha,Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa serikali za mitaa jijini Arusha, Wajumbe wa Jumuiya ya Maridhiano, viongozi kutoka Wizara ya Nishati, watendaji kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Masheikh kutoka taasisi mbalimbali za dini ya Kiislamu na wadau mbalimbali wa nishati safi nchini.