Watuhumiwa 23 wadakwa wizi wa bodaboda

DAR ES SALAAM: Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watu 23 kwa tuhuma za wizi wa pikipiki 39 maeneo mbalimbali ya Dar es salaam.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, SACP, Jumanne Muliro amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia mbinu ya kujifanya abiria na wakifika njiani hujitokeza watu wengine, ambao humtishia dereva kwa mapanga kumjeruhi na kumuibia pikipiki.

“Ufuatiliaji wa Jeshi la Polisi umebaini watuhumiwa hao baada ya kuziiba pikipiki wamekuwa wakiziuza kwa gharama nafuu mikoa mbalimbali, ikiwemo Mikoa ya Dodoma na Singida,” amesema Kamanda Muliro.

Amesema ufuatiliaji huo umefakiwa kukamata risiti mbalimbali kughushi za kusafirishia pikipiki za wizi, kadi  za usajili wa pikipiki za kughushi kadi  za usajili wa magari za kughushi, vyeti mbalimbali vya kuzaliwa na kimoja cha ndoa vya kugushi.

Pia wamekamata kitabu kimoja cha bima ya magari, nyaraka mbalimbali za TRA, barua mbalimbali zenye nembo za jeshi la Polisi Tanzania, mihuri mbalimbali ya Manispaa ya Kinondoni,Temeke, IIala, TRA, RITA, Mamlaka ya Bandari na mhuri wenye alama ya bibi na bwana.

Habari Zifananazo

Back to top button