Watumishi Moi wakumbushwa maadili, lugha za staha

Watendaji wa MOI wametakiwa kutoa lugha zenye staha kwa wagonjwa ambao ndio "mabosi" wao

DODOMA: WAFANYAKAZI wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamekumbushwa kufanya kazi kwa uadilifu, kutumia lugha za staha na kuzingatia maadili ya kazi.

Akifungua Kikao cha Pili cha Baraza la Sita la Wafanyakazi wa MOI, jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi hiyo Jijini hapa jana, Dk Marina Njelekela alisema kwa ujumla MOI inafanya kazi vizuri lakini wanatakiwa kuboresha katika maeneo hayo ili kusonga mbele zaidi.

“Kwa ujumla MOI inasonga mbele, lakini ili kufikia hatua ya juu zaidi wafanyazi wanatakiwa kufanya kazi kwa uadilifu zaidi na kutoa kauli nzuri kwa wateja,” alisema.

Dk Njelekela alisema watendaji wa MOI wanatakiwa kutoa lugha zenye staha kwa wagonjwa ambao ndio “mabosi” wao na kwa kauli nzuri wahitaji hao watakuja kwa wingi na watatoa fedha zaidi ambazo ndizo zinatumika kulipa mishahara.

Alisema anapokea taarifa kutoka kwa watu mbalimbali, wagonjwa wanaofika katika taasisi hiyo wangependa wahudumiwe na daktari bingwa au mbobezi tangu hatua ya kuingia, kulazwa hadi kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Katibu wa Baraza ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dk Mpoki Ulisubisya alisema mwenyekiti wa Bodi amewakumbusha wajibu wao kama viongozi na wafanyakazi lakini nao wamekuwa wakihimizana kutenda kazi kwa uadilifu, kutumia kauli njema na kuzingatii maadili.

Kuhusu vifaa ambavyo serikali imetoa katika kuboresha huduma za afya ikiwemo taasisi hiyo, Dk Mpoki alisema, wataendelea kukumbushana kama wafanyakazi ili kuhakikisha wanatumia vizuri vidumu kwa muda mrefu zaidi.

SOMA: Kairuki aahidi kuimarisha barabara, maji na ajira Kibamba 

Alisema mkutano wa baraza hilo pamoja na mambo mengine utaangalia maazimio ya mkutano uliofanyia Machi ili kuona ni namna gani bajeti iliyopangwa imetumika katika kutekeleza afua mbalimbali na kuweka malengo kwa ajili ya taasisi kusonga mbele.

Taasisi hiyo imejipanga kuendelea kutoa huduma bora zaidi kwa kuhudumia wagonjwa wa mifupa, ubongo na mgongo ili kusaidia wagonjwa wengi kupata huduma bora kwani wanavifaa, huduma za kibingwa na kibobezi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Dk Jane Madete aliwapongeza MOI kwa ushirikiano baina ya menejimenti na wafanyakazi na ndio maana taasisi hiyo inasonga mbele kihuduma.

Naye Mwenyekiti wa Tughe Tawi la Moi, Privatus Masula alisema mkutano huo pamoja na kupitisha bajeti pia utajadili changamoto za wafanyakazi katika kutekeleza kazi zao.

Hadio sasa katika tawi hilo kumekuwa na ushirikiano mzuri kati ya uongozi wa taasisi na wafanyakazi katika kupanga mipango na matumizi ya bajeti.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button