Wawili mbaroni kwa ubakaji
BUKOBA, Kagera: WANAUME wawili wanatarajiwa kufikishwa mahakamani na jeshi la polisi mkoani Kagera ili kujibu tuhuma zinazowakabili za matukio ya ubakaji kwa watoto.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo , Blasius Chatanda akizungumza leo amesema kuwa watuhumiwa hao wa ubakaji wanatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Amesema, jeshi hilo linaendelea na taratibu za kisheria dhidi ya watuhumiwa hao ambao ni Gaudiozi Rutayuga Yepa (42) mfanyabiashara wa simu katika mji wa Kayanga wilaya ya Karagwe na Philemon Reveliani (39) mkazi wa kisiwa cha Musira Manispaa ya Bukoba kwa tuhuma za ubakaji.
“Mtuhumiwa Rutayuga Yepa anadaiwa kutenda kosa la ubakaji Januari 02, mwaka huu majira ya saa 20:00 usiku katika mtaa wa Bomani, kata ya Kayanga, wilaya ya Karagwe ambapo alimrubuni mtoto mwenye umri wa miaka 10 mwanafunzi wa darasa la nne kwa kumwambia apande kwenye gari lake lenye namba za usajiri T 639 BKP aina ya pijoti ili ampeleke nyumbani kwao na baada ya mtoto huyo kupanda ndipo alimbaka kwa nguvu na kumsababishia maumivu makali mwilini”alisema Chatanda
Amesema mtoto huyo baada ya kurudi nyumbani na mama yake mzazi kuona alivyokuwa ameumizwa alimkimbiza hospitali ya Nyakahanga wilaya ya Karagwe kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kwa sasa hali yake inaendelea vizuri.
Alisema kuwa mtuhumiwa alikamatwa na kudhaminiwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kuanzia sasa kujibu tuhuma zinazomkabili.
Wakati huo huo, mtuhumiwa Philemon Revelian ambaye ni baba wa kambo wa mtoto aliyembaka mwenye umri wa miaka mitano anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 26, mwaka jana majira ya 09:00 asubuhi akiwa amebaki nyumbani na mtoto huyo katika kisiwa cha Msira kata ya Miembeni manispaa ya Bukoba baada ya mama mzazi wa mtoto huyo Gaudensia Charles (30) wakati ameenda katika kituo cha Afya Zamzam kwa ajili ya kujifungua.
Alisema baada ya kurudi nyumbani ndipo aligundua kuwa mtoto wake amebakwa na baada ya kugundua kuwa mtoto wake amebakwa na kufuatilia kwa kina zaidi ndipo aligundua kuwa, kitendo hicho kilifanywa na baba yake wa kambo ambaye ndiye mtuhumiwa.
Alisema mtoto anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoa wa Kagera,Bukoba na hali yake inaendelea vizuri na mtuhumiwa atafikishwa mahakamni mara tu upelelezi na taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Jeshi la polisi mkoa wa Kagera limeendelea kutoa onyo kwa watu wote wenye tabia hizo zilizo kinyume na maadili ya Kitanzania kuacha mara moja na halitasita kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote wenye tabia hizo na linawaomba wananchi wote kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha mkoa wa Kagera unaendelea kuwa salama.