Wazazi Mtwara wafundwa elimu kwa watoto

WAZAZI katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wametakiwa kuona umuhimu wa elimu kwa watoto kwa sababu ndio msingi pekee wa maisha ya watoto hao.

Akizungumza leo mkoani Mtwara wakati Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara ilipotembelea miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye halmashauri hiyo, Katibu wa CCM mkoani humo, Mobutu Malima amesema wazazi hao watumie fursa hiyo iliyoeletwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu watoto kupata elimu.

Kamati hiyo ya siasa mkoani huo ikiongozana na sekretarieti ya mkoa imetembelea miradi hiyo ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Hata hivyo miradi hiyo ya maendeleo iliyotembelewa kwenye halmashauri hiyo ni minne ikiwemo ujenzi wa nyumba ya mwalimu katika shule ya sekondari ya mkanaredi, ujenzi wa shule ya  mpya ya sekondari Kata ya Tandika.

Pia ujenzi wa madarasa matatu na matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Rahaleo pamoja na hospitali  ya halmashauri hiyo iliyopo mjimwema ambapo thamani ya miradi hiyo yote ni Sh bilioni 2.2.

Mobutu ameendelea kuwasisitiza wazazi na jamii kwa ujumla kuwa serikali inafanya uwekezaji mkubwa katika miradi hiyo ya elimu na mingine kwenye maeneo yao hivyo wanapaswa kuitumia fursa hiyo iliyoletwa na Rais huyo ili watoto waweze kupata elimu.

“Msingi wa maisha yoyote, urithi wa aina yoyote katika zama hizi ni elimu kwahiyo wapeni watoto elimu ili kuwajengea msingi wa maisha yao ya baadaye,”amesema Mobutu.

Sambamba na hilo, katibu huyo akiwa katika mradi wa ujenzi wa hospitali ya halmashauri hiyo iliyopo mjimwema amewasisitiza wasimamizi wa miradi kwenye manispaa hiyo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu miradi ili kuonyesha thamani ya fedha za miradi.

Mzazi na mkazi wa mtaa wa Tandika, Sada Makoko amepongeza uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika miradi ikiwemo ya elimu kwani majengo ni mazuri yanapendeza hivyo wazazi hao lazima waunge mkono jitihada hizo.

“Shule zinapofunguliwa tutajitahidi watoto waende shule na jinsi shule zilivyopendeza tunategemea kabisa ufaulu katika shule zetu hizi utakuwa mzuri na tutahakikisha tunachangia suala la chakula shuleni”amesema Sada

Habari Zifananazo

Back to top button